DAR-Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kinondoni, ACP Ally Wendo tarehe 10 Januari, 2026 amefanya kikao maalum na viongozi wa vikundi vya ulinzi shirikishi wa Wilaya ya Kimara chenye lengo la kuimarisha ulinzi na usalama, kurejesha amani na utulivu pamoja na kuwajengea uwezo askari katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza katika kikao hicho, ACP Wendo amesema lengo kuu ni kuvipa motisha vikundi ikiwemo kusikiliza changamoto zao na kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kudhibiti uhalifu.
Alisisitiza umuhimu wa ukamataji salama, utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu, pamoja na kusikiliza kero za wananchi kupitia Polisi Jamii.
“Polisi Jamii ni nguzo muhimu katika kulinda amani na usalama wa wananchi. Tunataka kufanya kazi kwa karibu nanyi, kuwasikiliza na kuhakikisha mnatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi, nidhamu na uadilifu,” alisema ACP Wendo.
Changamoto kubwa iliyotajwa ni kutokupata posho kutokana na wananchi wengi kugoma kuchangia ada ya ulinzi shirikishi.
Akijibu hoja hiyo, ACP Wendo aliahidi kushughulikia suala hilo kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, madiwani pamoja na watendaji wa serikali ili kutafuta utaratibu mzuri wa kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ulipaji wa ada ya ulinzi shirikishi.


