NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha masikitiko makubwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mwanasiasa mkongwe na mchumi mahiri, Mzee Edwin Isaac Mbilinyi Mtei, kilichotokea usiku wa Januari 19, 2026, jijini Arusha.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu leo Januari 20,2026 ambapo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba yake binafsi, Rais Dkt. Samia ametoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo mzito.
Rais Dkt.Samia amemkumbuka marehemu Mtei kama mmoja wa watumishi na viongozi waliotoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa, hususan katika sekta ya fedha, mipango na uchumi.
Ameeleza kuwa,marehemu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali muhimu, ikiwemo kuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania kati ya mwaka 1966 hadi 1974, na alikuwa miongoni mwa waasisi walioweka misingi ya uendeshaji wa Benki Kuu pamoja na kuimarisha uthabiti wa mfumo wa fedha nchini.
Pia, Rais Dkt.Samia ameeleza kuwa,marehemu Mtei ataendelea kukumbukwa katika historia ya siasa za vyama vingi nchini kama mmoja wa waasisi wa demokrasia ya ushindani wa vyama, na alitambuliwa kama mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Ameongeza kuwa,mchango wa marehemu utaendelea kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo, hususan kupitia maandiko yake binafsi (wasifu wa maisha) yanayoeleza safari yake ya maisha, fikra zake za kiuongozi na mchango wake katika kuijenga Tanzania ya kisasa.
Rais Dkt. Samia amewapa pole familia na wafiwa wote, akiwaombea faraja, nguvu na amani katika kipindi hiki kigumu, na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Edwin Mtei mahali pema peponi. Amina.
