Sadio Mané apeleka kilio Misri,Senegal yatinga fainali michuano ya AFCON

NA DIRAMAKINI

TIMU ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Senegal imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1–0 dhidi ya Misri.
Ni katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa leo Januari 14, 2026 katika dimba la Tangier Grand Stadium (Ibn Batouta Stadium) uliopo jijini Tangier, Morocco.

Bao hilo pekee la ushindi lilifungwa na mshambuliaji nyota wa Senegal, Sadio Mané, katika dakika ya 78 ya mchezo, baada ya kupokea pasi nje ya eneo la hatari na kupiga shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Misri, na kuamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wa Senegal walioufurika uwanjani.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa uliwashuhudia mabingwa hao wa Afrika wakionesha kiwango bora na nidhamu ya hali ya juu, huku wakidhibiti mchezo kwa kiasi kikubwa kuanzia kipindi cha kwanza hadi mwisho wa dakika 90.

Aidha,Senegal walionekana kuwa na mpango mzuri wa mchezo, wakimiliki mpira kwa muda mrefu na kuunda nafasi kadhaa hatari langoni mwa Misri.

Licha ya Misri kujaribu kusawazisha katika dakika za mwisho za mchezo, safu ya ulinzi ya Senegal ilionesha uimara na umakini wa hali ya juu, ikizuia mashambulizi ya wapinzani wao na kuhakikisha ushindi huo unadumu hadi filimbi ya mwisho.

Kwa matokeo hayo, Senegal sasa imejihakikishia nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika, wakisubiri kumkabili mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Nigeria na wenyeji Morocco.

Vilevile,ushindi huo umeongeza matumaini ya Senegal kutwaa taji la AFCON kwa mara nyingine na kuendelea kuthibitisha ubora wao katika soka la Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here