Utekelezaji wa Mfumo wa Anuani za Makazi (NaPA) ni hatua muhimu katika kuimarisha ukuaji wa huduma jumuishi za fedha nchini-Gavana Tutuba

DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa utekelezaji wa Mfumo wa Anuani za Makazi (NaPA) ni hatua muhimu katika kuimarisha ukuaji wa huduma jumuishi za fedha nchini, kwa kuwezesha kubaini maeneo yenye upungufu wa huduma za kifedha na kuchochea upanuzi wa huduma hizo kwa usawa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Gavana Tutuba aliyasema hayo wakati wa kikao chake na ujumbe kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ulioongozwa na Afisa Hesabu Mkuu kutoka Kitengo cha Uhasibu na Fedha, CFE Shakibu Mussa kilichofanyika Januari 14, 2026 katika ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, pande hizo zilijadiliana masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji na matumizi ya mfumo wa NaPA.

Alieleza kuwa mfumo huo utawezesha pia ufuatiliaji wa shughuli za kiuchumi kwa kuzingatia maeneo husika, pamoja na kuboresha upatikanaji wa takwimu sahihi na za kuaminika, zitakazosaidia katika upangaji na utekelezaji wa sera za fedha zinazolenga uhalisia wa uchumi wa taifa.
Aidha, Gavana alibainisha kuwa kupitia matumizi ya NaPA, benki zitakuwa na uwezo wa kufanya tathmini sahihi ya hatari za mikopo kwa kutumia taarifa za kijiografia za wakopaji, hatua itakayosaidia kupunguza mikopo chechefu na kuimarisha uthabiti wa sekta ya benki kwa ujumla.

NaPA ni mfumo wa kidijitali unaojumuisha kanzidata ya anuani za makazi, unaomwezesha mwananchi kupata taarifa muhimu kuhusu huduma mbalimbali zilizopo karibu na alipo, ikiwemo huduma za fedha.

Kupitia mfumo huu, mtumiaji anaweza kuwasiliana kwa urahisi na watoa huduma au kupata maelekezo ya namna ya kufikia huduma husika, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika matumizi ya mifumo ya kidijitali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here