UKISOMA Biblia utaona inatoa onyo kali dhidi ya uasherati na uzinzi, ikisisitiza kuwa ni dhambi zisizopaswa hata kutajwa miongoni mwa waumini.
Katika kitabu kitakatifu cha Waefeso 5:3, Mtume Paulo anawakumbusha watakatifu kuishi maisha ya utakatifu, wakijiepusha na uasherati,uchafu na tamaa zisizofaa.
Uasherati ni kujihusisha na tendo la ndoa kabla ya kufunga ndoa,ambapo uzinzi ni tendo la ndoa linalofanywa na mmoja wa wanandoa nje ya ndoa.
Biblia inabainisha kuwa,dhambi hizi ni za kipekee kwa kuwa hufanyika ndani ya mwili, kama inavyoelezwa katika kitabu cha 1 Wakorintho 6:18-19, na hivyo humharibu mtu binafsi na hekalu la Roho Mtakatifu.
Tofauti na dhambi nyingine, zinaa haisimamiwi kwa kuikemea bali kwa kuikimbia. Mfano wa Yusufu katika nyumba ya Potifa unaonesha nguvu ya uamuzi wa kumcha Mungu.
Licha ya kushawishiwa vikali, Yusufu alichagua kukimbia dhambi badala ya kuisaliti dhamiri na imani yake.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anabainisha kuwa,ni heri kukimbia kishawishi na kulinda utakatifu kuliko kukubali dhambi yenye madhara makubwa ya kiroho na kimwili.
1. Katazo la Neno moja, hilo la kwangu na lako,
Sisi sote kwa pamoja, linatuhusu tamko,
Ole kwa anayefuja, kwake hilo ni anguko,
USIZINI.
2. Ni amri yake Mungu, hiyo ni yangu na yako,
Ameiandika Mungu, kupuuza kusiweko,
Kwani hiyo huwa pingu, ya kuleta munganiko,
USIZINI.
3. Wakati dhambi zingine, wazitenda mbali huko,
Uzinzi huo uone, wakudhuru ndani yako,
Kwamba maroho mengine, wayavaa yawa yako,
USIZINI.
4. Kwamba wawaka tamaa, kwenye huo mwili wako,
Kwamba huwezi kukaa, una hiyo kiu yako,
Hadi kikombe kujaa, ndipo utulivu wako,
USIZINI.
5. Kumbe ufanyapo hivyo, hekalu la Mungu wako,
Linakuwa ni la hovyo, na kwako huyo hayuko,
Nawe waachwa ulivyo, uende gizani huko,
USIZINI.
6. Acha kuwaka tamaa, tumia nafasi yako,
Wanawake wamejaa, oa mpate wa kwako,
Kwa utakatifu kaa, chota kwa wakati wako,
USIZINI.
7. Mama una mume wako, huyo ni kisima chako,
Ni wa nini mchepuko, unachota dhambi huko,
Kwa huo uchafu wako, Muumba kwako hayupo.
USIZINI.
8. Kijana wewe kijana, kweli una nguvu zako,
Una mwili umenona, kakuumba Mungu wako,
Utakatifu ni zana, huo ni upako wako,
USIZINI.
9. Ukichochea mapenzi, kabla take muda wako,
Huo kwako ni udwanzi, tena doa kubwa sana kwako,
Pigo kwa chako kizazi, pia na uchaji wako
USIZINI.
10. Jinsi unajiachia, kujiuza mwili wako,
Ndivyo nuru yafifia, ya huo mvuto wako,
Kwa Mungu unatitia, na hata kwao wenzako,
USIZINI.
11. Kweli wavaa vizuri, na hivyo viwalo vyako,
Ukipita ng'aring'ari, kwa watu wa rika lako,
Kwa Mungu ona fahari, kuyashika maandiko,
USIZINI.
12. Wale wanazinizini, kwake Muumba hawako
Hata wakishika dini, ni kujidanganya huko,
Iingie akilini, uchafu Mungu hayuko,
USIZINI.
13. Hii amri si ombi, ni yangu tena ni yako,
Ukitaka weka kambi, kwamba Mungu aje kwako,
Hakikisha hii dhambi, haikumbatiwi kwako,
USIZINI.
14. Inapokusogelea, kukimbia pona yako
Kama waichekelea, jua itakula kwako,
Endapo ulilegea, muda fanya toba yako,
USIZINI.
15. Mungu utusaidie, tushike amri yako,
Dhambi isitufikie, ubaki utii kwako,
Kwa wakati utujie, tuyapate mema yako,
USIZINI.
16. Wewe unayejitunza, subiri malipo yako
Mungu tazidi kutunza, kwako udumu upako,
Muda wako utaweza, kumpa yule wako,
USIZINI.
(Kutoka 20:14)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767224602
