Serikali yahimiza ushirikiano na wadau wa sekta ya sanaa na utamaduni

ZANZIBAR-Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma, amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau wa sekta ya sanaa na utamaduni utasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya kudhibiti, kulinda na kutunza Utamaduni wa Mzanzibari.
Waziri Dkt. Riziki ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Utamaduni uliofanyika katika Ukumbi wa ZSSF Kariakoo, Wilaya ya Mjini, mkutano uliolenga kutoa maoni na changamoto zinazokabili sekta hiyo ili kuimarisha utamaduni wa Zanzibar.

Amesema iwapo Wazanzibari wataendelea kudumisha, kulinda na kutunza utamaduni wao wa asili, hatua hiyo italeta tija na mafanikio kwa jamii na Taifa kwa ujumla, sambamba na kuifanya Zanzibar kuendelea kutambulika kimataifa kupitia urithi wake wa kitamaduni.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mattar Zahor Masoud, ameahidi kuyafanyia kazi mapendekezo na changamoto zilizotolewa na wadau wa sekta hiyo kwa lengo la kukuza na kuimarisha sekta ya utamaduni nchini.

Amesema,utamaduni ni sehemu muhimu ya historia ya Taifa lolote duniani, hivyo unapaswa kulindwa kwa hali na mali ili uendelee kurithiwa na kizazi cha sasa na kijacho.

Wakitoa maoni yao, wadau wa sekta ya utamaduni wakiwemo Bi. Saada Hamad Ali kutoka Baraza la Wazee, Shehia ya Sharifumsa, pamoja na Bw. Faridi Hamid kutoka Taasisi ya Kusaidia Jamii, wameiomba Wizara ya Habari kufuatilia kwa karibu vijana wanaocheza na kupiga ngoma bila kufuata misingi na taratibu za utamaduni wa asili.

Wamesema kuwa, bila ya kuwepo kwa utamaduni wa asili, Taifa haliwezi kupiga hatua za maendeleo, hivyo wameomba kuendelezwa kwa utamaduni wa Mzanzibari ili uwe kivutio cha watalii na kichocheo cha kukuza uchumi wa nchi.

Mkutano huo wa wadau wa sekta ya utamaduni umehusisha taasisi mbalimbali zikiwemo Mabaraza ya Wazee, Wajasiriamali wa bidhaa za utamaduni, Wazee wa Mila pamoja na Matabibu wa Tiba Asili kutoka Wilaya sita za Unguja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here