NA GODFREY NNKO
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam imewakamata raia wawili wa China waliokuwa wakitafutwa kwa muda mrefu wakiwa na fedha haramu zaidi ya shilingi bilioni 2.
Picha na Mtandao.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Christian Nyakizee ameyabainisha hayo leo Januari 7,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari.
“Majina ya waliokamatwa ni Yao Licong na Wang Weisi ambao ni wakazi wa Oysterbay Phone Apartments, Kinondoni jijini Dar es Salaam. Walikamatwa wakiwa na fedha taslimu kiasi cha dola za Kimarekani 707,075 sawa na shilingi 1,732,333,750 pamoja na shilingi za Kitanzania 281,450,000 zikiwa ndani ya gari katika mifuko ya sandarusi.”
Amefafanua kuwa, fedha hizo zinashukiwa kuwa ni mazalia ya fedha zilizotakatishwa kupitia taarifa za kadi za kibenki zilizoibiwa kutoka kwa watu mbalimbali nje ya nchi.
“Watuhumiwa hao wameshindwa kuthibitisha uhalali wa upatikanaji wa fedha hizo, kwani hawana kampuni au biashara halali zilizowapatia kiasi tajwa na hawana uthibitisho (stakabadhi) wa namna walivyonunua fedha za kigeni walizokutwa nazo,”amefafanua Mkuu huyo.





