DAR-Ujumbe kutoka Benki Kuu ya Kenya (CBK) ulioongozwa na Naibu Gavana wake, Dkt. Susan Koech, umetembelea ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam tarehe 13 January 2026 kwa lengo la kujifunza kuhusu Mpango wa Ununuzi wa Dhahabu unaotekelezwa na BoT.
Ujumbe huo ulipokelewa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anayesimamia Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, ambaye aliwaeleza wageni hao kuwa mpango huo unaohusisha unuzi wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo wa wakubwa umeleta mafanikio makubwa katika kuongeza hifadhi ya fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania.
Kwa upande wake, Dkt. Susan Koech ameishukuru BoT kwa kukubali kuwapokea na kuwapa fursa ya kujifunza kuhusu mpango huo, akieleza kuwa BoT imekuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa dhahabu.
“Tumejionea mageuzi makubwa yaliyofanywa na BoT katika mpango wa ununuzi wa dhahabu pamoja na mafanikio yake. Nakumbuka katika mkutano wa Kamati ya Masuala ya Fedha (Monetary Affairs Committee-MAC) unaojumuisha Benki Kuu za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, BoT ilipewa jukumu la kuzisaidia nchi nyingine katika ukanda huu katika utekelezaji wa mpango huu,” alisema Dkt. Koech.
Kufuatia kuanza kutekelezwa kwa Sheria ya Madini, kifungu cha 59, kuanzia tarehe 1 Oktoba 2024 hadi tarehe 13 Januari 2026, jumla ya tani 17.916 za dhahabu zenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 2.44417 zimekwishanunuliwa.






