ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kufanikisha ujenzi wa viwanja vya michezo katika kila Wilaya, pamoja na ujenzi wa Viwanja vya Mikoa kwa Unguja na Pemba.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Januari 13,2026 katika Uwanja wa Michezo wa Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba, wakati wa Uzinduzi rasmi wa Uwanja huo uliokwenda sambamba na Mchezo wa Fainali ya Michuano ya Kombe la Mapinduzi kati ya Azam FC na Yanga SC za Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kazi kubwa na nzuri ya kusimamia ujenzi wa viwanja hivyo, akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukuza sekta ya michezo, kuibua vipaji vya vijana na kuimarisha afya pamoja na mshikamano wa kijamii.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru wadhamini wote wa Michuano ya Kombe la Mapinduzi, wakiongozwa na Mdhamini Mkuu Benki ya NMB, kwa kufanikisha mashindano hayo maalum yanayolenga kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar na kuendeleza michezo hususan soka.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza wananchi wa Pemba kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia Mchezo wa Fainali kati ya Azam FC na Yanga SC, akieleza kuwa ushiriki huo mkubwa ni kielelezo cha uzalendo na kuthamini mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika mchezo huo wa Fainali, Klabu ya Yanga African imefanikiwa kulitwaa Kombe la Mapinduzi baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya Azam FC, baada ya timu hizo kutoka sare dakika tisini za mchezo. Yanga SC imezawadiwa Shilingi Milioni 150 za Ubingwa pamoja na Kombe la Mapinduzi, tuzo iliyokabidhiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Uzinduzi na mchezo huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa michezo, viongozi wa vyama vya michezo pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya Zanzibar na Tanzania Bara.






















.jpg)
.jpg)
.jpg)