Wazabuni 2,000+ wapigwa msasa matumizi ya NeST

DAR-Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) zimeendesha mafunzo kwa wazabuni zaidi ya 2,000 juu ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kielektroniki (NeST) katika mikoa minne tofauti.
Wazabuni waliopatiwa mafunzo hayo wanatoka katika mikoa minne ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na Mbeya. Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yalijikita katika maeneo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake, wajibu wa wazabuni katika ununuzi wa umma na uuzaji wa bidhaa kwa kutumia NeST.

Maeneo mengine ni majadiliano (negotiations) kwa kutumia mfumo wa NeST, kuwasilisha dhamana ya utekelezaji wa mkataba, kuomba malipo ya utekelezaji wa mkataba pamoja na uwasilishaji wa malalamiko na rufaa katika zabuni za umma.
Akifungua mafunzo hayo ya siku moja jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Denis Simba amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wazabuni kuhusu mfumo wa NeST ili waweze kuondokana na changamoto zilizokuwa zinawakabili wakati wa kuomba zabuni za umma.

Aidha, Bw. Simba amesema kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 imeweka upendeleo maalum kwa wazabuni wa ndani ambapo miradi yote yenye thamani ya shilingi bilioni 50 inatakiwa kutekelezwa na wazabuni Watanzania (wazawa).

“PPRA ina uhakika wa kusimamia vizuri sheria hii ya ununuzi wa umma na kuhakikisha kuwa mfumo huu wa NeST ili kuwapa fursa na kuwarahisishia kufanya kazi kwa haraka na wepesi zaidi...kwa hiyo wazabuni nawasihi kutumia fursa ya mafunzo haya vyema ili kupata uelewa mpana wa mfumo huu wa NeST,” amesema Bw. Simba

Bw. Simba ameongeza kuwa mfumo wa NeST umeweka mazingira rafiki kwa wazabuni, PPRA inatoa wito kwenu kutekeleza wajibu wenu kwa uadilifu, kuzingatia sheria na kanuni za ununuzi wa umma. Kwa kutumia mfumo, Mamlaka imeweza kuondoa janja-janja nyingi ambapo imesaidia Serikali kupata thamani ya fedha katika miradi mbalimbali.
“Nawasihi kuzingatia sheria, epukaneni na kona-kona nyingi zisizo na manufaa kwenu na ununuzi wa umma kwa ujumla, mfumo wetu kwa sasa umeunganishwa ‘intergrated’ na mifumo mingine kama vile Brela, Muce n.k. hivyo na nawahakikishia kuwa hivi karibuni tutaondokana na changamotoya ucheleweshaji wa malipo kwa wazabuni,” amesema Bw. Simba

Naye Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Huduma za Sheria PPAA, Bi. Florida Mapunda amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wadau wa ununuzi wa umma kuhusu matumizi ya moduli ya usimamizi wa malalamiko na rufaa kielektroniki katika mfumo wa NeST.

“Kwa sasa Sheria ya Ununuzi wa Umma imeweka sharti la lazima kwa ununuzi wa umma kufanyika kwa njia ya Kieletroniki kupitia mfumo wa NeST. Kutokana na sharti hilo, PPAA kwa kushirikiana na PPRA tumejenga moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST ili kuwasaidia wadau wa ununuzi kuwasilisha malalamiko na rufaa kieletroniki,” amesema Bi. Mapunda.

Bi. Mapunda aliongeza kuwa, moduli imerahisisha zoezi la uwasilishaji wa malalamiko yatokanayo na michakato ya ununuzi wa umma pamoja na kusaidia utunzaji wa kumbukumbu za taarifa za malalamiko na rufaa ambazo zitakuwa zinawasilishwa katika michakato yote ya ununuzi wa umma.
Mafunzo hayo ya siku moja kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST yamefanyika tarehe 10 Januari 2026 katika Mikoa ya Dar es Salaam kwa wazabuni zaidi ya 500, Dodoma wazabuni zaidi ya 500 walipatiwa mafunzo hayo, Mwanza wazabuni 500 na Mbeya zaidi ya wazabuni 500 lengo likiwa ni kuendelea kutoe elimu kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here