TANGA-Katika jitihada za kuimarisha ustawi wa wananchi na kukuza uchumi wa Taifa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza katika elimu ya fedha kwa kuandaa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika mkoani Tanga, yakilenga kuwajengea wananchi nidhamu na uelewa wa matumizi sahihi ya huduma za kifedha.
Maadhimisho hayo, yanayoandaliwa na Wizara ya Fedha, yatafanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga kuanzia Januari 19 hadi 26, 2026, na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).
Lengo kuu ni kuwawezesha wananchi kuongeza kipato, kupunguza umaskini na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia matumizi jumuishi ya huduma rasmi za fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, alisema kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21–2029/30, unaolenga kuijenga sekta ya fedha iliyo imara, shirikishi na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Alisema kuwa katika wiki hiyo, wananchi watapata fursa ya kushiriki katika maonesho ya huduma na bidhaa za kifedha, semina, machapisho ya elimu ya fedha, pamoja na kupata taarifa kupitia majukwaa ya kidigitali, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Bi. Mjema alibainisha kuwa utoaji wa elimu ya fedha kwa umma ni eneo la kipaumbele la Serikali, hivyo Wizara ya Fedha iliandaa Programu ya Kutoa Elimu ya Fedha kwa Umma ya mwaka 2021/22–2025/26 inayotekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha nchini.
Aliongeza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na wadau, imeandaa Nyenzo ya Kufundishia Elimu ya Fedha inayojumuisha mada muhimu kama usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo, uwekezaji, bima, bima ya amana, kodi na hatifungani, kwa lengo la kuwajengea wananchi uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Aidha, alisema Serikali imelenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, takribani asilimia 80 ya Watanzania wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Utafiti wa FinScope wa mwaka 2023, ni asilimia 53.5 tu ya nguvu kazi nchini iliyotumia huduma rasmi za fedha, hali inayoonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika mifumo rasmi ya kifedha.
Katika kufanikisha maadhimisho hayo, Wizara ya Fedha itashirikiana na Wizara, Idara na Wakala za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wasimamizi wa sekta ya fedha, taasisi za fedha, sekta binafsi, asasi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari, taasisi za elimu na utafiti pamoja na taasisi za dini zinazotoa huduma za kifedha.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi,” ikilenga kuhamasisha wananchi kutumia huduma rasmi za kifedha, kujiwekea akiba, kukopa kwa tija na kulipa madeni kwa wakati. Serikali imesisitiza kuwa elimu na huduma zote zitakazotolewa katika Wiki ya Huduma za Fedha ni bure bila gharama yoyote.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Noves Moses, alisema kuwa washiriki wa maadhimisho hayo watapata elimu kuhusu uwekezaji katika dhamana za Serikali, usimamizi wa fedha binafsi na namna ya kuwasilisha malalamiko dhidi ya taasisi za fedha pale huduma zinapokosa ubora.
Alieleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania imeanzisha mfumo wa kidigitali wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha ujulikanao kama “SEMA BoT,” unaowezesha wananchi kuwasilisha na kutatuliwa kwa malalamiko yao kwa ufanisi.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanatarajiwa kuwafikia makundi mbalimbali yakiwemo watumishi wa umma, wanafunzi, wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalumu, wajasiriamali wadogo na wa kati, waandishi wa habari, watoa huduma za fedha pamoja na umma kwa ujumla, huku yakiwa chachu ya kuongeza uelewa wa haki, wajibu na nidhamu ya kifedha kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
