DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameshiriki mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Wang Yi, na Serikali ya Tanzania, uliofanyika jijini Dar es Salaam, uliojadili namna ya kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia), akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Wang Yi, baada ya kikao kati ya Serikali ya Tanzania na Waziri huyo, kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kilicho jadili namna ya kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.

Mheshimiwa Wang Yi aliyewasili nchini leo, alikuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, mazungumzo ambayo yalilenga kuimarisha uhusiano wa kimkakati kwa kuendeleza miradi ya maendeleo yenye maslahi ya nchi hizo mbili.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisema kuwa miongoni mwa ajenda walizojadili ni pamoja na bandari, kuboresha Reli ya TAZARA, yenye urefu wa kilomita 1860 kutoka Tanzania hadi Zambia.
Mhe. Balozi Kombo alitaja maeneo mengine waliyojadiliana na kukubaliana kushirikiana yalikuwa kuendeleza program za elimu kwa vijana 300 kwenda kusoma China, kuimarisha ushirikiano wa kisasa na kidiplomasia, kiuchumi, kijamii, miundombinu na uhusiano wa watu kwa watu wa nchi hizo mbili.
Aidha aliongeza kuwa eneo la biashara lilijadiliwa ambapo kiwango cha biashara kinatakiwa kuongezeka kati ya nchi hizo mbili ambapo hivi sasa biashara kati ya China na Tanzania imefikia thamani ya shilingi bilioni 9 kwa mwaka.
Watanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa ya ushirikiano wa Tanzania na China kwa kuongeza mauzo ya nje kwa kuongeza uzalishaji wa asali, parachichi maharage ya soya.
Alisema kuwa eneo lingine ambalo China itawekeza Tanzania, ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa mtandao wa intaneti wa 5G hadi vijijini ili kukuza matumizi ya mitandao huo kwa manufaa ya wananchi pamoja na kulegeza masharti ya upatikanaji wa visa ya watu wanaoingia na kutoka katika nchi hizo mbili.
Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, ambapo kwa mwaka 2024, thamani ya biashara kati ya Tanzania na China ilifikia takriban dola za Marekani bilioni 5.2.
Kampuni za China pia zimeendelea kuwekeza nchini katika sekta za viwanda, kilimo, huduma, usafirishaji, mawasiliano na utalii, ambapo Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ilisajili miradi ya China 343 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1 na kuzalisha ajira 82,404.
Tanzania na China pia zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya miundombinu ya uchukuzi ambapo reli ya TAZARA ni moja wapo ya alama ya urafiki na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.






