NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Watu wa China imeonesha utayari wa kuongeza nafasi za ufadhili wa masomo kwa Watanzania kutoka 300 na kuendelea, kwa mwaka ili kuwapa uwanda mpana wa kwenda kuongeza ujuzi wa taaluma mbalimbali nchini China.
Hayo yamebainishwa leo Januari 9,2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi ambaye amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Amesema, katika mazungumzo hayo wamezungumzia nafasi za masomo kwa sababu ni miongoni mwa programu zake, ambayo anaendelea nayo ya kuwaombea Watanzania nafasi za masomo katika ngazi mbalimbali kuanzia digrii ya kwanza, ya pili hadi ya tatu.
Pia, pande hizo mbili zimekubaliana kukamilisha taratibu zote za ndani ambazo zilikuwa zimebakia ili kurahisisha masuala ya anga na kuweka wepesi kwa upande wa Visa, ni ili Watanzania wakitaka kwenda China wasikumbane na ugumu ambao wanakumbana nao wakati upande wa Wachina wakija nchini hawakumbani na changamoto nyingi kwa upande wa Visa.
Waziri Kombo amesema, raia wa China akifika uwanja wa ndege nchini anapata Visa, hivyo na Tanzania inataka wakubaliane ili mambo yawe mepesi kidogo kutokana na uzito au ugumu ambao Watanzania wanakumbana nao wakitaka Visa ya China.
Licha ya jitihada hizo, Waziri Kombo ametoa raia kwa Watanzania, pale jambo hlo litakapofanikiwa kuhakikisha wanazingatia vigezo na masharti vya Visa, hatua ambayo itawaondolea vikwazo hasa wale ambao huwa wakisafiri wanazidisha muda na kukumbana na adhabu.
Mheshimiwa Waziri Kombo, pia ameishukuru Serikali ya China kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania, hususan katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu, afya, elimu, nishati na viwanda.
Pia,ameeleza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya China katika kuvutia uwekezaji, biashara na teknolojia kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Naye Mheshimiwa Wang Yi ameeleza, utayari wa China wa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake za maendeleo, na kusisitiza kuwa China itaendelea kuwa mshirika wa kuaminika wa Tanzania na Afrika nzima katika kutekeleza ajenda za maendeleo ya pamoja ikiwemo kupitia Mpango wa Ukanda wa njia (Belt and Road Initiative) na Jukwaa la Ushirikiano wa Afrika na China (FOCAC).
Ziara ya Waziri huyo inalengo kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya China na Tanzania, ikiwa China ni mshirika mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania.
Katika hatua nyingine,Waziri Kombo amesema, katika mazungumzo yao ambayo yamefanyika kirafiki na kindugu, Wachina wameipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukamilisha Uchaguzi Mkuu, huku wakitoa pole kwa yaliyotokea Oktoba 29 na baada ya uchaguzi.
Aidha, wamewahimiza Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha amani yao ambayo ni nguzo muhimu katika kujiletea maendeleo binafsi, kijamii na Kitaifa.
Pia, Waziri Kombo amesema, kupitia mazungumzo na Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa China amegusia mambo mbalimbali ambayo yanaongeza na kuimarisha ushirikiano zaidi baina ya pande hizo mbili.
“Tumezungumzia suala la reli ya TAZARA, kuimarishwa ili kuwa ya kisasa na unaweza kutumia muda ule ule ambao unaenda Dodoma kufika Lusaka (Zambia) na suala la bandari.”
Aidha, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa China ameeleza kuwa, suala la reli ya TAZARA linawagusa zaidi Wachina, kwani imebeba historia kubwa na wakati wanaijenga reli hiyo China haikuwa na uwezo ambao inao kwa sasa, lakini kwa kile kidogo ambacho walikuwa nacho walijitolea kwa ajili ya TAZARA wakati huo.
“Pia, kuna wananchi wao (Wachina) wadogo kabisa Mheshimiwa Wang Yi ameeleza wenye umri mdogo kabisa, wengine miaka 20 na walikuwa hawajaoa bado walifariki na makaburi yao yapo kama kumbukumbu, kwa hiyo Serikali ya Watu wa China imeamua kwa makusudi mradi ule (TAZARA) kuupa hadhi ya juu kama kumbukumbu ya waliopoteza roho zao, wale wajenzi waliopoteza roho zao kwa ajili ya kuzisaidia nchi hizi mbili, Tanzania na Zambia.”
