NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeshiriki katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (IFEM) kwa mujibu wa Sera yake ya Ushiriki katika soko hilo ya mwaka 2023, hatua iliyolenga kuongeza ukwasi wa fedha za kigeni nchini.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 4,2026 na Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika ushiriki huo, Benki Kuu imeuza Dola za Marekani milioni 47.25 kupitia mnada wa ushindani, kwa kiwango cha wastani cha kubadilisha fedha cha Shilingi 2,561.44 kwa Dola moja ya Marekani.
Aidha, kwa mujibu wa matokeo ya mnada huo, kiasi kilichotangazwa awali kilikuwa Dola za Marekani milioni 30. Hata hivyo, kutokana na mahitaji ya soko, kiasi kilichowasilishwa pamoja na kilichokubaliwa kilifikia Dola milioni 47.25.
Mnada huo ulihusisha jumla ya benki 29, na benki zote zilizoshiriki ziliibuka washindi, hali inayoonesha ushindani mzuri na mahitaji makubwa ya fedha za kigeni katika soko.
Pia,viwango vya ushindani vilionesha kuwa, kiwango cha juu cha ubadilishaji kilikuwa Shilingi 2,610 kwa Dola moja, huku kiwango cha chini kikiwa Shilingi 2,538. Aidha, viwango vya juu na vya chini vilivyokubaliwa vilibaki katika kiwango hicho hicho.

