Gavana Tutuba atoa rai kwa benki kuu za SADC

ARUSHA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amezitaka Benki Kuu za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuimarisha usalama wa mifumo ya TEHAMA na uthabiti wa kiutendaji ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali na kuhimili hatari zinazojitokeza.
Akifungua kikao cha Kamati Ndogo ya Magavana wa Benki Kuu za SADC leo Februari 23,2026, Gavana Tutuba alisema kuwa, mazingira ya uendeshaji wa Benki Kuu yameendelea kubadilika kwa kasi, yakichochewa na maendeleo ya haraka ya teknolojia, ongezeko la mashambulizi ya kimtandao, pamoja na matarajio makubwa ya umma ya upatikanaji endelevu na wa uhakika wa huduma za kifedha.
Alieleza kuwa kaulimbiu ya kikao hicho, “Benki Kuu Zilizojipanga kwa Mustakabali: Teknolojia, Usalama na Uhimilivu katika Vitendo,” inaakisi umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya usimamizi wa vihatarishi ili kuhakikisha uwekezaji wa TEHAMA unaendana na malengo ya kimkakati ya taasisi.

Gavana Tutuba alieleza kuwa kuongezeka kwa ustadi wa wahalifu wa mtandao kunahatarisha miundombinu muhimu ya kifedha na kuhimiza ushirikiano wa kikanda katika kubadilishana taarifa na kujiandaa kwa pamoja kukabiliana na vitisho hivyo.
Kuhusu teknolojia zinazoibukia, alibainisha kuwa matumizi ya Akili Unde (AI) na uchambuzi wa takwimu yanaweza kuongeza ufanisi katika usimamizi na uangalizi wa sekta ya fedha, lakini akasisitiza kuwa matumizi hayo lazima yaambatane na misingi ya maadili, utawala thabiti na udhibiti madhubuti wa hatari.

Akizungumzia mafanikio ya BoT, Gavana Tutuba alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Benki Kuu imeboresha miundombinu ya TEHAMA, kuimarisha usalama wa mifumo ya msingi na kuongeza uwezo wa kurejesha huduma wakati wa dharura.
Hatua hizo, alisema, zimeongeza uthabiti na uaminifu wa huduma za fedha nchini na kuendana na viwango vya kikanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here