ZANZIBAR-Kampuni ya mawasiliano ya Halotel Tanzania kupitia tawi lake la Zanzibar imetoa hundi ya shilingi milioni 10 kwa Taasisi ya Majlis Al Maarifa Islamiya kwa ajili ya kutekeleza mpango wa uzalishaji wa vifaa vya usalama barabarani.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika ofisi za kampuni hiyo Maisara, Mjini Unguja, ambapo Ofisa kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Sajenti Staff (SSGT) Ali Abdalla Juma, alisema msaada huo ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Alisema takwimu za ajali zinaonesha bado kuna changamoto, hivyo upatikanaji wa alama na vibango vya tahadhari utasaidia kupunguza hatari, hususan katika maeneo yenye msongamano wa watu.
“Vibango na vizibao vya usalama vinamkumbusha dereva kupunguza mwendo na kusimama ili kupisha watembea kwa miguu. Wakati mwingine madereva huendesha wakiwa na msongo wa mawazo, hivyo alama hizi ni kinga muhimu,” alisema Sajenti Ali.
Aliongeza kuwa, kupitia hatua hiyo, Halotel imejidhihirisha kama mdau anayeshika hatamu katika kusaidia kampeni za usalama barabarani, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi liko tayari kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha ajali zinapungua.
Aidha, aliwataka waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kutii sheria za barabarani na kuwakumbusha watumiaji wote wa barabara kutimiza wajibu wao.
“Endapo kila mmoja atachukua hatua stahiki, ajali nyingi zinaweza kuepukika,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara wa Halotel Tanzania, Abdallah Salum, alisema kampuni hiyo imeamua kuwekeza katika mpango huo kwa kutambua kuwa usalama wa wananchi ni jukumu la pamoja.
"Tunalenga kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watumiaji wa barabara."
Alieleza kuwa vifaa vitakavyozalishwa ni pamoja na alama za barabarani, vibango vya tahadhari na vizibao maalum (safety bibs) kwa mabalozi wa usalama barabarani, vitakavyosaidia kudhibiti mwendo wa magari na kulinda watembea kwa miguu.

