Mbolea yatajwa kuwa silaha ya kuinua uchumi wa Babati

MANYARA-Wakulima katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara wametakiwa kuachana na kilimo cha mazoea na kuanza kutumia mbolea kwa kuzingatia ushauri wa wataalam na matokeo ya upimaji wa afya ya udongo ili kuongeza tija na kubadilisha maisha yao.Wito huo umetolewa Februari 25,2026 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo kwa wataalamu wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo na taasisi zake ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya Mali Shambani mkoani Manyara.

Amesema kuwa uchumi wa halmashauri hiyo unategemea kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo, ambapo wakulima hulima mazao mbalimbali ikiwemo mahindi, ufuta, alizeti, mbaazi, dengu, ngano, viazi na mviringo.
"Wakulima wetu wamekuwa wakiamini zaidi matumizi ya samadi kuliko mbolea za viwandani,"ameongeza kuwa wakulima wakihamasika na kupokea elimu uzalishaji utaongezeka.

Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe amesema, Mamlaka imebaini kuwa wakulima wengi wanalima kwa mazoea bila kuzingatia kanuni za matumizi sahihi ya mbolea na kueleza Mamlaka imeendelea kuwahamasisha wakulima kupima afya ya udongo ili wajue ni mbolea gani inafaa kwa mashamba yao badala ya kutumia mbolea kwa mazoea.

Raphael Paulo, mkulima wa mahindi, vitunguu na viazi kutoka Kijiji cha Nar, amesema matumizi sahihi ya mbolea yanaongeza kipato kwa kiasi kikubwa.

"Bila kutumia mbolea unaweza kupata magunia nane tu, lakini ukitumia kwa usahihi unaweza kupata magunia 25 au zaidi. Hii inaongeza pato la mkulima mmoja mmoja,” amesema na kutoa wito kwa wakulima wenzake kupokea ushauri wa wataalam na kutumia pembejeo kwa usahihi.

Naye Martha Alexandra, mkulima wa mahindi na vitunguu, amesema wakulima wamezoea kutumia aina moja ya mbolea kwa mazoea bila kujali mahitaji halisi ya udongo.

“Sasa tumeelekezwa tusikariri mbolea na tuzingatie ushauri wa wataalam ili kilimo chetu kiwe cha kisasa na chenye tija,” amesema.
Taasisi chini ya Wizara ya Kilimo zinazoshiriki kampeni hiyo ni pamoja na , Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Taasisi ya Kuthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania ( TOSCI), Mamlaka ya Afya ya mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) pamoja na kampuni mbalimbali za mbegu na mbolea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here