DODOMA-Wizara ya Fedha imewakutanisha Wakuu wa Vitengo vya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma, cha kujadili changamoto zinazokwaza utekelezaji wa masharti ya Vifungu vya 56 hadi 60 vya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 vinavyohusiana na masuala ya upendeleo wa Kitaifa, upendeleo wa kipekee kwa watu au Kampuni za Ndani, ushiriki wa kampuni za ndani na watalaamu katika mikataba ya Ushauri Elekezi.
Sheria hiyo pia inahusu Matumizi ya Wataalamu wa ndani katika mikataba ya kazi za ujenzi na huduma zisizo za kitaalamu, upendeleo kwa bidhaa za ndani, kujenga uwezo wa watu na kampuni za ndani, uingiaji wa ushirika au mikataba midogo na kampuni za ndani, umiliki wa mtaji wa hisa, pamoja na upendeleo kwa Makundi Maalum ya Kijamii.
Kikao hicho kililenga kupendekeza mbinu bora za utekelezaji wa vifungu hivyo ili kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za ununuzi wa umma na ugavi.
Katika kikao hicho, washiriki walijadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410, pamoja na vikwazo vinavyoathiri ushiriki wa makampuni ya ndani, makundi maalum ya kijamii na wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) katika shughuli za mnyororo wa ugavi nchini.
Aidha, kupitia kikao hicho mapendekezo mbalimbali yalitolewa ili kuimarisha ushiriki wa makundi hayo katika shughuli za mnyororo wa ugavi.
Kikao hicho kiliwahusisha Wakuu mbalimbali wa Idara na Vitengo vya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo: Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu; Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI; Wizara ya Fedha; Wizara ya Nishati; Wizara ya Uchukuzi; Wizara ya Ujenzi; Wizara ya Madini; Benki Kuu ya Tanzania (BOT); Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA); Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Umma (PPAA); Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA); Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF); na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).











