NA DIRAMAKINI
MIRAMBO Yusuf amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kujizolea kura 257 katika Mkutano Mkuu wa dharura uliofanyika usiku wa kuamkia Jumapili katika Ukumbi wa Lekham jijini Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo, mpinzani wake mkuu, Othman Omar Dunga, alipata kura 177.
Kufuatia kutangazwa kwa matokeo, Dunga alieleza wasiwasi wake kuhusu uhalali wa baadhi ya wajumbe walioshiriki katika mkutano huo, akidai kuwa kwa mtazamo wake, si wote waliokuwa na sifa stahiki za kupiga kura.
Mirambo, ambaye kabla ya ushindi huo alikuwa Mwenyekiti wa chama Wilaya ya Kigoma Mjini, anakuwa Mwenyekiti wa nne wa CUF, akichukua nafasi iliyoachwa na Ibrahim Lipumba.
Katika kinyang’anyiro hicho, mgombea wa tatu, Nkunyunyika Siwale, alipata kura 6 kati ya kura 448 zilizopigwa, huku kura nyingine sita zikiharibika.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Miraji Mtibwiliko aliibuka mshindi kwa kupata kura 264, akiwashinda Mohammed Ngulangwa aliyepata kura 88 na Mussa Mbarouk aliyepata kura 82.
Kwa upande wa Zanzibar, nafasi ya Makamu Mwenyekiti imechukuliwa na Haroub Mohamed Shamsi aliyepata kura 256, akimshinda Mbarouk Seif Salim aliyepata kura 171.
Awali, Amina Rashid Salim alikuwa amejitoa katika kinyang’anyiro hicho kabla ya upigaji kura kuanza.
Uchaguzi huo unaashiria mwanzo wa sura mpya ya uongozi ndani ya CUF, wakati chama hicho kikikabiliwa na jukumu la kuimarisha mshikamano wa ndani na kujenga imani miongoni mwa wanachama wake.
Hata hivyo, hoja ya uhalali wa baadhi ya wajumbe imeendelea kuwa mjadala, hali inayoweza kuathiri taswira ya mchakato huo iwapo haitapatiwa ufumbuzi wa kina kupitia vikao halali vya chama.
