PWANI-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt.Alphonce Temba ambaye pia ni mwanasiasa machachari na mfanyabiashara mwenye maono makubwa, ameendelea kudhihirisha karama na neema kubwa aliyopewa na Mungu nchini, hususan akiwa miongoni mwa wanakijiji wa Vigwaza kwa Zoka na Kambini.
Mwanamaendeleo huyo ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa mbele ya jamii,kila anapopata kipaza sauti katika hadhara huzungumza hoja zenye mvuto na mashiko kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Akiwa anafananishwa na hayati Mchungaji Christopher Mtikila, Dkt.Temba amejijengea umaarufu mkubwa kupitia ushiriki wake katika vipindi mbalimbali vya kijamii, kiuchumi na kisiasa katika vyombo vya habari, ikiwemo TBC 1, ITV na vinginezo.
Februari 16, 2026, katika ziara ya Mbunge wa Chalinze, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, iliyoendelea katika jimbo lake kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumpa kura za kishindo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kufanikisha ushindi wa Uchaguzi Mkuu 2025 pamoja na yeye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Chalinze, Dkt. Temba alijitokeza kwa mchango na hoja mbalimbali za maendeleo.
Dkt.Temba alijiunga na Kata ya Vigwaza mwaka 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kukubali ushauri wake kupitia barua aliyomuandikia ya kuhamisha mzani wa magari wa Kibaha Maili Moja na kujengwa Vigwaza Kambini na wazo la ujenzi wa Bandari Kavu.
Wazo hilo lilitokana na maono yake ya mbali, akiwa ameishi katika mataifa 12 tofauti duniani.
Alipofika Kata ya Vigwaza aliomba ardhi katika Kijiji cha Ruvu Darajani, ambapo alipewa ekari tisa pamoja na watu wengine saba.
Serikali ya Kijiji cha Ruvu Darajani iliweka sharti la kujenga Kituo cha Afya (zahanati) kabla ya Mkutano Mkuu wa Kijiji kuwaridhia kumiliki ardhi hiyo. Mkutano huo ulifanyika mwaka 2009 katika Ofisi za Kijiji cha Ruvu Darajani.
Kutokana na ushawishi wake na maelezo yake kuhusu ujio wa bandari kavu na mzani wa malori ya mizigo ambao ungetanua fursa na kuinua uchumi wa ukanda huo, Mkutano Mkuu ulimchagua Dkt.Temba kuwa Mwenyekiti wa Wawekezaji huku Mzee Abdhuli akichaguliwa kuwa Katibu.
Chini ya uongozi wake, waliandaa mikutano ya wawekezaji waliokuwa wakiishi jijini Dar es Salaam, wakikutana katika Hoteli ya Ubungo Plaza.
Ndani ya miezi sita walifanikiwa kujenga na kukamilisha Kituo cha Afya cha Kijiji cha Ruvu Darajani, kujenga baadhi ya madarasa ya Shule ya Msingi Ruvu Darajani na kuingiza umeme pamoja na nguzo kadhaa.
Katika Kijiji cha Vigwaza kwa Zoka, Dkt.Temba amewaleta wawekezaji kutoka China wanaojenga viwanda 32 pembezoni mwa reli kuelekea Tanga, ambapo hadi sasa viwanda vitano vimekamilika na kuanza kazi.
Aidha,alitoa msaada wa shilingi milioni 1.5 kupiga plasta Ofisi ya Kijiji na Kitongoji cha Vigwaza kwa Zoka. Mwaka 2025, wakati wa kampeni za Mbunge na Diwani, alikichangia chama bendera za CCM kupamba Kata nzima ya Vigwaza.
Kwa sasa ni Mwenyekiti wa Mbala Kisambi City, mpango unaolenga kushirikisha wananchi na wahamiaji kujenga mji wa kisasa kwa pamoja kwa kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo na kupanga mji huo kitaalamu.
Mpango huo unajumuisha maeneo makubwa ya kibiashara, maeneo ya maziko ya kisasa, masoko ya mazao Mbala ili kupunguza mazao yanayoelekezwa Dar es Salaam pamoja na usimamizi wa taka za kilimo kama maranda yanayotumika kubebea nyanya, majani ya migomba kwa ajili ya kubebea maparachichi na ndizi.
Majani hayo yakifika Dar es Salaam hutupwa hovyo na wakati wa mvua ukwama katika madaraja na kusababisha mafuriko au kuleta magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu na magonjwa ya ngozi.
Katika hatua za awali, chini ya uongozi wake, barabara ya zamani kutoka Mbala hadi Kisambi Shule yenye urefu wa kilomita saba imechongwa na mpango unaendelea kuifikisha Mnarani, Magulumatale na Buyuni.
Vitongoji vya Mbala Kisambi vinatajwa kuwa katikati ya Bandari Kavu ya Kwala (Kibaha Vijijini) na Bandari Kavu ya Bagamoyo.
Aidha,katika mkutano wa wananchi uliofanyika Februari 16, 2026, Mbunge Ridhiwani Kikwete alimkaribisha Dkt.Temba kuchangia ujenzi wa Ofisi ya CCM Kata ya Vigwaza baada ya Mbunge huyo kuchangia matofali 500.
Dkt.Temba alimshukuru Mbunge na kuwahamasisha wananchi kuthamini maendeleo waliyonayo, akisema katika Mkoa wa Pwani ni vigumu kupata kata yenye maendeleo kama ya Vigwaza.
Aliahidi kuchangia lori la kokoto kuanzia ujenzi huo na kuruhusu malori yake kubeba kifusi bure kutoka kwenye chimbo lake lenye leseni Vigwaza kwa Zoka kwa ajili ya kutengeneza mandhari ya zahanati kubwa yenye zaidi ya ekari tano.
Mbunge alitoa maelekezo kwa Mganga Mkuu kuhakikisha wananchi wanaanza kupata huduma ndani ya siku moja huku vyumba vilivyobaki na sakafu vikikamilishwa.
Aidha, alikosoa mandhari ya nje ya zahanati na kuagiza ipandwe miti ili kuongeza mvuto. Kauli hiyo ilimfanya Dkt.Temba kuahidi kusambaza kifusi bure, wananchi wakigharamia mafuta tu.
Akijenga hoja kwa ujasiri, Dkt.Temba alisisitiza kuwa zahanati hiyo lazima ifanane na hadhi ya Mbunge na hadhi ya wana Vigwaza.
Katika mkutano huo, hoja ya majengo ya TRA ya ukaguzi yaliyokamilika zaidi ya miaka minne iliyopita lakini hayajaanza kutumika iliibuliwa.
Dkt.Temba aliwakumbusha wananchi kuwa viongozi mbalimbali, wakiwemo Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, waliwahi kuahidi kushughulikia suala hilo bila mafanikio.
Alimwomba Mbunge Ridhiwani Kikwete “kupewa mfupa mgumu” ili aukwamue mkwamo huo. Mbunge aliahidi ndani ya siku mbili atakutana na wahusika na kulifanyia kazi jambo hilo, kauli iliyopokelewa kwa shangwe.
Katika mkutano huo, Mbunge aliwasifu viongozi wa CCM Kata ya Vigwaza akiwemo Mwenyekiti Athumani Kumuyi, Katibu Amiri Dunga na Diwani Ramadhani Kirumbi (Komi), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Ujenzi wa Mali ya Halmashauri ya Chalinze, kwa mchango wao katika kuifanya Vigwaza kuwa ngome imara ya CCM ndani ya Jimbo la Chalinze.
Chalinze inaelezwa kuwa moja ya ngome imara za Chama Cha Mapinduzi zenye matokeo makubwa katika chaguzi za vyama nchini.
Mbunge huyo aliambatana na Mstahiki Meya wa Chalinze, Mheshimiwa Leoni Mgweno, ambaye alikiri kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kufika Vigwaza na kushangazwa na kasi ya maendeleo. Mbunge alieleza wazi imani yake kwa Diwani Komi na kumtaka asiangushe matarajio ya wananchi.
Baadhi ya wananchi, akiwemo Omari Athumani wa Visezi na Mama Abuu wa Vigwaza Sekondari, walimpongeza Dkt.Temba kwa uthubutu wake wa kuhoji masuala ya maendeleo, wakisema wamefarijika na ahadi ya Mbunge kukutana na TRA.
Mwaka huu, Dkt.Temba alifanya ziara nchini Kenya na Uganda ambako alishauri juu ya umuhimu wa miungano ya viongozi wa nchi, ikiwemo ujio wa Rais Yoweri Museveni kukutana na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kujadili kuondolewa kwa vikwazo vya mipakani, hoja iliyoungwa mkono na wadau mbalimbali.
Kwa ujumla,Dkt.Alphonce Temba ameendelea kujidhihirisha kama kiongozi mwenye ushawishi, maono na uthubutu katika kusukuma ajenda za maendeleo ya Vigwaza na maeneo jirani, huku akibaki kuwa sauti ya wananchi katika majukwaa mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.Soma kwa kina hapa》》》

