DAR-Stendi Kuu ya Daladala Mbezi Luis, wilaya ya kipolisi Kimara Kata ya Msigani, imekuwa kitovu cha elimu na ulinzi baada ya Polisi Kata na wadau wa Polisi jamii kushughulikia kero ya upandishaji holela wa nauli kwa abiria, hususani nyakati za usiku.
Akizungumza katika tukio hilo lililofanyika tarehe 06 Februari 2026, Mkaguzi Joseph Kamala, Polisi Kata ya Msigani, alitoa elimu kwa madereva na abiria kuhusu madhara ya tabia hiyo na kusisitiza kuwa upandishaji holela wa nauli ni kosa la jinai kama makosa mengine ya kisheria.
Jumla ya watu 111 walinufaika na elimu hiyo, wakiwemo madereva 29 na abiria 82. Mbali na suala la nauli, elimu ya miradi mitano ya ushirikishwaji jamii ilitolewa ikihusisha usalama barabarani, utoaji wa taarifa sahihi za uhalifu kwa wakati, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kina mama na watoto, kutii sheria bila shuruti, pamoja na elimu dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.
Abiria walihimizwa kutoa taarifa mara moja wanapokutana na vitendo vya upandishaji holela wa nauli au uhalifu mwingine wowote, huku madereva wakikumbushwa wajibu wao wa kuzingatia sheria na kulinda haki za wasafiri.
Katika hitimisho,Polisi Kata Insp. Kamala alibainisha kuwa eneo la Mbezi Luis linakusanya watu wengi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji, hivyo akaomba operesheni za mara kwa mara ziende sambamba na elimu kwa jamii, pamoja na uwepo wa askari wa usalama barabarani hasa nyakati za jioni, ili kukomesha kabisa vitendo hivyo.

