Serikali yasisitiza umuhimu wa PPP utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

DAR-Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na Sekta binafsi ili kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo inatekelezwa na kuboresha huduma muhimu ikiwemo usafiri ili kurahisisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Hayo yameelezwa na Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPU), Bw. Bashiru Taratibu, wakati akifungua kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Kikao cha Kwanza cha ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha kupitia Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPU), Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) Tanzania na Wizara ya Kazi na Uwekezaji-Zanzibar, kupitia Idara ya ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPD).

Alisema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi hivyo ni muhimu Serikali kuendelea kutoa fursa za uwekezaji kwa Sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuboresha miundombinu na miradi mingine ya maendeleo ili kukuza uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya Watanzania.
"Dira ya 2050, utekelezaji wake unaanza Juni 2026 na Mpango wa nne wa maendeleo ambapo ndio utakuwa Mpango wa kwanza unaotekeleza Dira hiyo umeitaka sekta binafsi kuchangia asilimia sabini ya utekelezaji wa Mpango huo, PPP tuhakikishe kuwa kunakuwa na miradi ya maendeleo ambayo sasa tutawakaribisha sekta binafsi. Alisema Bw. Taratibu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Uwekezaji, Zanzibar, Bw. Rashid All Salim, alizitaka Sekta mbalimbali kutekeleza jukumu lao la kuandaa miradi ya maendeleo ili kutoa fursa kwa Sekta binafsi kuitekeleza miradi hiyo.

‘’Sekta ndio wana miradi ikiwemo sekta ya ujenzi, afya, kilimo, sekta ya miundombinu, kwa hiyo tunatoa wito kwa sekta zitayarishe miradi na maandiko ya miradi inayouzika ili tuweze kuiuza kwa wawekezaji,’’ alisema Bw. Salim.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), Bw. David Kafulila, alitaja maeneo mbalimbali ambayo sekta binafsi inaweza kuwekeza ili kuleta maendeleo kiuchumi. ​

‘’Muelekeo huo wa Serikali kuhakikisha kwamba sekta binafsi inashiriki sehemu kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya maji, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, bandari na reli, ni sehemu muhimu ya kujenga uchumi mkubwa wa ushindani utakaofikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,"alisema Bw. Kafulila.
Kikao cha Kwanza cha ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha Tanzania Bara na Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar katika masuala ya PPP kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar Es Salaam kiliambatana na ziara ya wajumbe kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa Tanzania Bara kwa utaratibu wa PPP ikiwemo Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), pamoja na Mradi wa DDC jijini Dar Es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here