MARA-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Wilaya ya Bunda mkoani Mara imesaidia hospitali kuongeza mapato kutoka shilingi 800,000 hadi shilingi milioni 4 kwa siku.
Hayo yamebainishwa Februari 19,2026 wakati wa warsha ya TAKUKURU na wadau wa sekta ya Afya iliyofanyika wilayani Bunda.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Dkt.Andrew Masamu ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (kulia) amesema kuwa, kabla ya uchambuzi wa mfumo wa kielektroniki wa utoaji huduma za matibabu uliofanywa na TAKUKURU, hospitali hiyo ilikuwa inapata mapato ya shilingi 800,000 hadi shilingi 1,500,000 kwa siku.
Baada ya TAKUKURU kufanya uchambuzi na kutoa mapendekezo ya mapungufu yaliyobainika mapato yamepanda na kufikia shilingi 3,000,000 hadi 4,000,000 kwa siku.
Aidha, ameipongeza TAKUKURU kwa kazi hiyo ambayo imesaidia mapato ya Hospitali kuongezeka na hivyo kuongeza tija katika utoaji huduma kwa wananchi wilayani hapo.
Vilevile amewahimiza wadau wengine wanaotoa huduma kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU wakati wowote kwa manufaa ya jamii wanayoihudumia.
