DAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema, Mashindano ya 22 ya Kimataifa ya Quraan Tajweed ni jukwaa muhimu la kuimarisha mapenzi ya Quraan, kukuza vipaji vya vijana na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia taaluma ya usomaji wa Quraan.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Februari 28, 2026 katika fainali ya mashindano hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Khidmatul Quran Tanzania na kufanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam, yakihusisha washiriki kutoka mataifa 12.Ameipongeza Taasisi ya Khidmatul Quran kwa kuendeleza mashindano hayo kwa kiwango cha kimataifa, akieleza kuwa yana mchango mkubwa katika kujenga kizazi chenye maadili, hofu ya Mwenyezi Mungu na nidhamu ya kiroho.
Aidha, amewapongeza washiriki wote kwa ustadi wao na kuwashukuru wadhamini, hususan Benki ya CRDB kupitia kitengo cha Al Barakah.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wadhamini na waumini kuchangia miradi ya Taasisi hiyo ikiwemo ujenzi wa Skuli ya Quraan na Kituo cha masomo ya Dini ya Kiislamu.
Katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza alikuwa Bilal Seif kutoka Misri (97%) aliyepata Dola za kimarekani 5,000, akifuatiwa na Muhammad Hussein kutoka Malaysia (90%) aliyepata Dola 3,000, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Hassan Kesi kutoka Tanzania Bara (89.5%) aliyepata Dola za kimarekani 2,000.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, mabalozi, viongozi wa dini, wadhamini na wananchi mbalimbali.




























