MANYARA-Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara tarehe 26 Machi,2026 imemtia hatiani aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Sukuro, Bw. Daud Samson Ndagala, katika shauri la Jinai Na. 4344/2026 kwa makosa mawili ya uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, kosa la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu wa mali ya umma kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (Marejeo ya mwaka 2023). Kosa la pili ni kuchepusha mali kinyume na kifungu cha 29 cha sheria hiyo.
Ilielezwa mahakamani kuwa, mshtakiwa akiwa katika nafasi yake ya uongozi kama Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Sukuro, alitumia vibaya dhamana aliyopewa kwa kufanyia ubadhirifu fedha kiasi cha shilingi 1,083,000.
Fedha hizo zilitokana na mauzo ya mifuko 57 ya saruji iliyokuwa imekusudiwa kutumika katika ukarabati wa zahanati hiyo.
Aidha, mshtakiwa alikutwa na hatia ya kuchepusha tofali 220 zilizokuwa zimeletwa kwa ajili ya mradi huo wa ukarabati, ambapo aliziuza kwa mtu binafsi kwa jumla ya shilingi 605,000, na hivyo kusababisha vifaa hivyo kutotumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Mheshimiwa Charles Uisso, ambaye alieleza kuwa mshtakiwa alikiri makosa hayo baada ya kufikia makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Kutokana na makosa hayo, mahakama ilimhukumu mshtakiwa kifungo cha nje cha miezi sita, pamoja na amri ya kurejesha fedha zote alizofanyia ubadhirifu kiasi cha shilingi 1,688,000 kwa mhanga, ambaye ni Zahanati ya Sukuro.
Ilielezwa kuwa, hadi wakati wa kusomwa kwa hukumu, mshtakiwa alikuwa tayari amerejesha kiasi cha shilingi 845,000 katika akaunti ya benki ya Zahanati ya Sukuro iliyopo Benki ya NMB. Mahakama iliamuru kiasi kilichosalia cha shilingi 843,000 kilipwe kabla au ifikapo tarehe 26 Julai 2026.
Shauri hili liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Kituo Maalum cha Mererani, Bw. Gervas Sarakikya.
.jpeg)