NA DIRAMAKINI
KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), katika kikao chake kilichofanyika Machi 17, 2026, imepitia mwenendo wa ligi pamoja na matukio mbalimbali yaliyojitokeza na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya vilabu, waamuzi, wachezaji na mashabiki.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 19,2026 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Matukio ya Ligi Kuu ya NBC
Katika mchezo namba 72 uliochezwa kati ya Singida BS FC na Young Africans SC uliomalizika kwa ushindi wa mabao 3-0 kwa Young Africans, shabiki wa klabu hiyo, Carlos Leonard Mayangura, amefungiwa kwa muda wa miezi 12 baada ya kubainika kuongoza kundi la mashabiki na baadhi ya maofisa wa ulinzi kuvunja madirisha ya chumba cha kuvalia na kusababisha uharibifu.

Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Aidha, klabu ya Young Africans imetozwa faini ya Shilingi milioni tano na kutakiwa kugharamia matengenezo ya uharibifu uliofanywa na mashabiki wake, kwa mujibu wa Kanuni ya 47 (1 & 3).
Katika mchezo namba 111 ambapo Simba SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida BS FC, mwamuzi wa kati Katanga Hussein kutoka Tabora amefungiwa mizunguko mitatu kwa kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria za mchezo.
Ilielezwa kuwa, mwamuzi huyo alishindwa kutoa maamuzi sahihi baada ya kipa wa Simba, Djibrilla Kassali, kumfanyia rafu mchezaji wa Singida BS, Joseph Guede ndani ya eneo la penati. Hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Kwa upande mwingine, klabu ya Singida BS imetozwa faini ya Shilingi milioni tano kutokana na meneja wa timu hiyo, Othmen Najjar, kushindwa kuvaa sare rasmi za timu kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:8 ya Taratibu za Mchezo.
Katika mchezo namba 104 uliowakutanisha Azam FC na Young Africans SC na kumalizika kwa sare ya bila kufungana, klabu ya Azam imetozwa faini ya Shilingi milioni tano kwa kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na badala yake kutumia korido, kinyume na Kanuni ya 17:20.
Pia, mwamuzi wa kati Ally Mnyupe kutoka Morogoro amefungiwa mizunguko mitatu kwa kosa la kushindwa kutafsiri sheria baada ya kushindwa kutoa uamuzi sahihi kufuatia rafu iliyofanywa na mchezaji wa Azam, Fuentes Mendoza, dhidi ya mchezaji wa Young Africans, Prince Dube ndani ya eneo la penati.
Vilevile, klabu ya Young Africans imepigwa faini ya Shilingi milioni tano kufuatia mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi baada ya kumalizika kwa mchezo huo.
Hatua kwa Ligi ya Championship
Katika Ligi ya Championship, klabu ya Kagera Sugar imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuwasili katika kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM), kinyume na Kanuni ya 17:2.
Wachezaji wa klabu hiyo, David Luhende na Erasto Nyoni, wametozwa faini ya Shilingi milioni moja kila mmoja kwa kosa la kumwaga kimiminika uwanjani wakati wa ukaguzi wa awali wa uwanja wa Ushirika, Kilimanjaro.
Aidha, mchezaji Andrew Vincent wa Kagera Sugar amefungiwa michezo mitatu pamoja na kutozwa faini ya Shilingi milioni moja kwa kumpiga ngumi mchezaji Tunga Said wa Polisi Tanzania.
Kwa upande wa klabu ya Stand United, imetozwa faini ya Shilingi milioni mbili baada ya mashabiki wake kuwarushia mawe na kutoa vitisho kwa waamuzi, hali iliyosababisha kusimamishwa kwa mchezo kutokana na hofu ya usalama.
Mbali na hayo, katika mchezo namba 168 kati ya Barberian FC na Mbeya Kwanza FC uliomalizika kwa sare ya bila kufungana, mwamuzi wa kati Haji Mtandohima kutoka Mtwara amefungiwa mizunguko mitatu kwa kushindwa kutafsiri sheria za mchezo.
Hitimisho
TPLB imesisitiza umuhimu wa kuzingatia nidhamu, sheria na taratibu za uendeshaji wa ligi ili kulinda hadhi ya mashindano hayo.
Hatua zilizochukuliwa zinalenga kuhakikisha haki, usalama na uadilifu vinaendelea kudumishwa katika soka la Tanzania.