NA DIRAMAKINI
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, imetoa maamuzi mbalimbali ya kinidhamu kufuatia matukio yaliyojitokeza katika michezo ya hivi karibuni ya Ligi Kuu ya NBC.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB leo Machi 27,2026.
Katika mchezo namba 85 uliowakutanisha Pamba Jiji FC na Simba SC, uliomalizika kwa sare ya mabao 1-1, klabu ya Simba imepigwa faini ya shilingi milioni 10.
Adhabu hiyo imetokana na mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wa mchezo huo walipokuwa wakielekea vyumbani baada ya kumalizika kwa mechi.
TPLB imeeleza kuwa, hili ni kosa la pili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, baada ya tukio kama hilo kuripotiwa Februari 25, 2026 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Kwa mujibu wa kanuni za ligi, hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia Kanuni ya 47:1 kuhusu udhibiti wa klabu kwa makosa ya mashabiki.
Katika mchezo namba 110 kati ya TRA United FC na Young Africans SC uliomalizika kwa sare ya bila kufungana, klabu ya TRA United imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya shilingi 500,000.
Adhabu hiyo imetolewa kutokana na wachezaji wake kuonyeshwa jumla ya kadi sita katika mchezo huo, ikiwemo zaidi ya tano zinazoruhusiwa kwa mujibu wa kanuni. Hatua hiyo imezingatia Kanuni ya 47:10 ya Ligi Kuu.
Aidha, katika mchezo namba 126 uliowakutanisha Mtibwa Sugar FC na Young Africans SC (1-1), mchezaji wa Yanga, Djigui Diarra, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya shilingi milioni 2 kwa kumshambulia mwamuzi wa kati baada ya mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Tukio hilo limeelezwa kuwa ni kinyume cha Kanuni ya 41:5(5.3) inayohusu udhibiti wa wachezaji.
Mbali na adhabu hiyo, Diarra pia ametozwa faini nyingine ya shilingi milioni 2 kwa kuonesha ishara isiyo ya kiungwana (kidole cha kati) kuelekea mashabiki, kitendo kilichofanyika wakati akitoka uwanjani baada ya mechi.
Katika hatua nyingine, mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Gilbert Mrina kutoka Kilimanjaro, amesimamishwa kuchezesha mechi za ligi kwa muda baada ya kubainika kufanya maamuzi yenye utata, ikiwemo kushindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya tukio la kumshambulia mwamuzi.
Awali, mwamuzi huyo alikuwa tayari ameshaadhibiwa kwa kufungiwa mechi tatu kufuatia makosa ya awali katika mchezo kati ya Mbeya City FC na Namungo FC.
Pia, mwamuzi msaidizi namba mbili, Abdulaziz Ally kutoka Arusha, amefungiwa mechi tano kwa kosa la kushindwa kutafsiri vyema sheria za mpira wa miguu.
Tukio hilo lilijitokeza dakika ya 36 aliporuhusu bao ambalo lilipaswa kukataliwa kutokana na mchezaji kuwa katika nafasi ya kuotea, kabla ya Pacome Zouzoua kufunga bao hilo.
Aidha,TPLB imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia nidhamu kwa ukali ili kulinda hadhi ya ligi na kuhakikisha sheria zinafuatwa ipasavyo.
