DAR-Mkazi wa Ocean Road jijini Dar es Salaam, Hamid Ahmed Hussein, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na jumla ya mashtaka 43, yakiwemo ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.
Mashtaka hayo yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Franco Kiswaga, ambapo Wakili wa Serikali, Cathbet Bilinyi, alidai kuwa mtuhumiwa alijihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka, kutumia nyaraka za uongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.
Upande wa mashtaka ulieleza kuwa kati ya Januari 2020 na Februari 2026, mtuhumiwa alighushi stakabadhi na hati za malipo akidai zimetolewa na Manispaa ya Temeke, hali ambayo si ya kweli.
Kupitia mbinu hiyo, anadaiwa kujipatia fedha kutoka kampuni binafsi kiasi kinachofikia shilingi bilioni tano.
Aidha, katika shtaka la utakatishaji fedha, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alifanya miamala ya kifedha kwa lengo la kuficha asili ya fedha zinazodaiwa kupatikana kwa njia haramu.
Hakimu Kiswaga amesema kuwa, kosa la utakatishaji fedha halina dhamana, na mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo katika hatua ya sasa.
Kwa upande wa utetezi, wakili Josephat Mabula ameiomba mahakama izingatie haki ya mtuhumiwa, akieleza kuwa amekaa mahabusu kwa siku 23 tangu kukamatwa kwake.
Mahakama imeelekeza upelelezi ukamilishwe kwa haraka, huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Aprili 9, 2026 kwa ajili ya kutajwa tena
