BoT kuanzisha kampuni ya udhamini wa mikopo kukuza upatikanaji wa mitaji na ajira

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza mpango wa kuanzisha kampuni ya udhamini wa mikopo (Credit Guarantee Corporation) kwa lengo la kupanua upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara, kuchochea ajira na kukuza sekta binafsi nchini, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamesemwa leo Machi 30,2026 katika makao makuu ndogo ya BoT jijini na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Mabenki na Viongozi wa Taasisi za Kifedha kwa mwaka 2026.

Gavana Tutuba amesema kuwa, kampuni hiyo inalenga kuziba pengo la upatikanaji wa dhamana kwa waombaji mikopo, hususan wale wasio na mali za kuweka rehani.

Ameeleza kuwa,kupitia mpango huo, wadau mbalimbali wa maendeleo, ikiwemo Benki ya Dunia, wamekubali kuunga mkono jitihada hizo kwa kuongeza rasilimali fedha.

Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, kiasi cha dola za Marekani milioni 150 kinatarajiwa kuongezwa na Benki ya Dunia kupitia Serikali ikiwa ni mkopo nafuu.

“Tunatarajia kuanzisha kampuni itakayosaidia kurasimisha biashara, kuwawezesha wajasiriamali kuandaa maandiko ya miradi yenye vigezo vinavyokubalika na taasisi za fedha, pamoja na kufuatilia uwezo wao wa kukopesheka,” amesema Gavana Tutuba.

Ameongeza kuwa,kampuni hiyo pia itakuwa na jukumu la kutoa dhamana kwa waombaji mikopo wasiokuwa na mali, iwe ni zinazohamishika au zisizohamishika, hatua inayotarajiwa kuongeza ushiriki wa makundi mbalimbali ya wananchi katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, BoT inaendelea na mchakato wa mapitio ya mifumo na sheria ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa kutumia nyaraka mbadala, ikiwemo vyeti vya taaluma. Hatua hiyo inalenga kuwajumuisha vijana wengi wanaohitimu elimu ya juu, lakini wanakosa sifa za kupata mikopo kutokana na ukosefu wa dhamana.

Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, muundo wa kampuni hiyo utajumuisha idara maalum zitakazoshughulikia utoaji wa dhamana pamoja na uandaaji wa maandiko ya miradi.

Amebainisha kuwa, waombaji watakaokosa maandiko ya miradi watapatiwa msaada wa kitaalamu ili kuboresha mawazo yao na kuyageuza kuwa miradi yenye tija na inayokubalika kifedha.

Katika hatua nyingine, BoT imeeleza kuwa, kampuni hiyo inatarajiwa kuwa huru katika uendeshaji wake, huku benki kuu ikibaki na jukumu la usimamizi na utoaji wa leseni kwa kuzingatia misingi bora ya utawala na maendeleo endelevu.

Sambamba na hilo, amesema BoT imeendelea kuimarisha programu za elimu ya fedha kupitia Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kupata ujuzi wa kuandaa maandiko ya miradi na kusimamia rasilimali fedha kwa ufanisi.

Kupitia chuo hicho kilichopo Mwanza, mitaala miwili ya elimu ya fedha imeandaliwa, ikijumuisha mtaala wa ndani ya mfumo rasmi wa elimu na ule wa nje ya mfumo huo.

Gavana Tutuba amebainisha kuwa,utekelezaji wa mitaala hiyo umeanza kuleta matokeo chanya, hususan kwa wanawake walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu ambao wameweza kunufaika na mafunzo hayo.

Ameongeza kuwa, taasisi mbalimbali zimeanza kupeleka wataalamu wao, hususan wanawake, katika chuo hicho kwa ajili ya mafunzo zaidi, huku BoT ikiendelea kubuni mifumo na mikakati mipya ya kuhakikisha elimu ya kifedha inawafikia Watanzania wengi zaidi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here