Rais Dkt.Samia apokea ripoti za CAG,TAKUKURU na PPRA, asisitiza uwajibikaji na ulinzi wa rasilimali za Taifa

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Machi 30,2026 amepokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taarifa ya Utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Taarifa ya Mwaka ya Tathmini ya Utendaji Kazi wa Ununuzi wa Umma, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

Rais Dkt.Samia amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu na usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma, akieleza kuwa misingi hiyo ni nguzo muhimu katika kuimarisha utendaji wa Serikali na kuharakisha maendeleo ya Taifa.

Aidha, Rais Dkt.Samia amepongeza kazi inayofanywa na taasisi hizo katika kuimarisha uwazi na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, akisema juhudi hizo zinaendelea kulinda rasilimali za Taifa kwa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

"Nimesikiliza taarifa zilizowasilishwa na taasisi zetu, na ninaendelea kusisitiza kuwa uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma si jambo la hiari, bali ni wajibu wa msingi kwa kila kiongozi na mtumishi wa umma," amesema Rais Dkt.Samia.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Charles Kichere akisoma Muhtasri wa Ripoti yake kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 kutoka kwa Bw. Charles Kichere, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

Akiizungumzia Ripoti ya CAG, Rais Dkt. Samia amesema tathmini hiyo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma, akibainisha kuwa Serikali imepokea na itazifanyia kazi hoja za ukaguzi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wa ripoti za TAKUKURU na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Rais Dkt.Samia amesema zimeonesha hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, kuongeza uwazi katika manunuzi ya umma na kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Bw. Crispin Chalamila akisoma Muhtasari wa Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

Aidha,amepongeza Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), akisema umeongeza uwazi na ushindani katika manunuzi ya Serikali, sambamba na kuagiza kuimarishwa kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi na ufuatailaji wa matumizi ya rasilimali za umma.

"Tuendelee kuimarisha mifumo ya kidigitali ili kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma."

Rais pia amekemea vitendo vya uzembe, ubadhirifu na matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali za umma, akionya dhidi ya vitendo vya makusudi vinavyokwamisha juhudi za maendeleo ya Taifa.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba akisoma Muhtasari wa Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Bw. Dennis Simba, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

“Kila kiongozi na mtumishi wa umma ana wajibu wa kuhakikisha rasilimali za Taifa zinasimamiwa kwa uadilifu, kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya nchi yetu.”

Aidha, Rais amezitaka taasisi za umma kuchukua hatua kwa wakati kushughulikia hoja zilizobainishwa katika ripoti za ukaguzi, ili kuimarisha uwajibikaji, kulinda rasilimali za Taifa na kuongeza ufanisi wa Serikali katika kuwahudumia wananchi.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonesha kuwa,deni la Taifa linaendelea kuwa himilivu, likizingatia uwezo wa Serikali kulihudumia pamoja na mwenendo wa ukuaji wa uchumi na mapato ya ndani.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Ripoti hiyo pia imebainisha ongezeko la hati safi kwa taasisi za umma, hali inayoashiria kuimarika kwa uwazi na usimamizi wa rasilimali za umma.

Kwa upande wa ununuzi wa umma, Taarifa ya Mwaka ya Tathmini ya Utendaji Kazi wa Ununuzi wa Umma imewasilishwa kwa Rais, ikilenga kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here