DODOMA-Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema kuwa gharama za kufanya vipimo vya vinasaba vya binadamu (Human DNA) zimeongezeka kutoka shilingi 100,000 kwa sampuli moja hadi kufikia shilingi 212,000 kutokana na gharama za mchakato wa vipimo hivyo.
“Gharama kwa sampuli moja ni shilingi 212,000. Kwa kesi ya baba, mama na mtoto gharama inazidisha mara tatu. Gharama zinazobaki zinapaswa kulipwa na Serikali ya Tanzania, kwani awali ilipaswa kuwa shilingi 70,000 mpaka shilingi 80,000 kwa sampuli moja,” alisema Dkt. Mafumiko.
Dkt. Mafumiko alitoa kauli hiyo Machi 11, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari Maelezo, uliopo katika jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Aliongeza kuwa, ongezeko la gharama linatokana na mchakato wa vipimo vya DNA, likiwemo matumizi ya vifaa maalumu, kemikali na rasilimali za kiufundi zinazohitajika ili kuhakikisha matokeo ni sahihi na yanayoweza kutumika kisheria.
Pia,taarifa hiyo inabainisha kuwa, kwa kesi zinazohusisha baba, mama na mtoto, gharama zinazidishwa mara tatu kutokana na idadi ya sampuli zinazohitajika.
Aidha,hii inatokana na umuhimu wa vipimo hivyo katika kesi za kisheria, uhalifu na masuala ya urithi, ambapo matokeo sahihi ni muhimu sana.
