PWANI-Jeshi la Polisi Mkoani Pwani limetoa taarifa kuhusu vifo vya watu wanne waliouawa kwa kukatwa mapanga katika klabu ya pombe za kienyeji iliyopo Kata ya Kiwangwa wilayani Bagamoyo.
Tukio hilo limetokea Machi 12, majira ya saa 2:45 usiku, ambapo mtuhumiwa wa mauaji hayo, Boniphace Ndalemi (53), maarufu kama Swai, anadaiwa kuwashambulia wateja sehemu za vichwani baada ya kuzuka kwa mzozo wa kifedha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, katika taarifa yake Machi 14/2026 ,ameeleza kuwa awali mtuhumiwa alifika siku hiyo klabuni hapo saa 11 jioni kunywa pombe aina ya ‘Mabuya’ na kuondoka.
Hata hivyo, alirejea saa 2:15 usiku na kuanza kudai Sh5,000 kwa mmiliki wa klabu hiyo, Asha Athman, akidai aliacha fedha hizo awali.
Mzozo ulipamba moto baada ya mmiliki huyo kukanusha kupewa fedha hizo, jambo lililopelekea wateja wengine kuingilia kati kutoa msaada, ambapo mtuhumiwa alianza kuwashambulia kwa panga na kusababisha Vifo vya watu wanne.
Watu waliouawa katika shambulio hilo wametambuliwa kuwa ni Mwajisumbua Ramadhani (mkazi wa Mwetemo),Omary Seif (mkazi wa Msoga),Ijumaa Mrisho (mkazi wa Miono) na Kibwenzi (jina moja lililotambulika).
Baada ya Jeshi la Polisi kufika eneo la tukio, mtuhumiwa alikaidi amri ya kujisalimisha na kuendelea kuhatarisha usalama wa askari na raia ambapo ili kumdhibiti, askari walilazimika kumpiga risasi ya mguu wa kulia, lakini alifariki dunia akiwa njiani kuelekea Kituo cha Afya Kiwangwa kwa matibabu.
Kamanda Morcase ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi au serikali za mitaa wanapoona viashiria vya uhalifu ili kuzuia maafa kama hayo.
.jpeg)