Historia mpya Tanzania, TRC yaanza kuunda vichwa vya treni za MGR nchini

DAR-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imetoa wito kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania wanaounda na kukarabati vichwa vya treni za MGR, kwa kuwapa mafunzo thabiti ndani na nje ya nchi ili kuongeza maarifa, stadi na ubunifu katika utendaji wa kazi hiyo.
Wito huo umetolewa leo Machi 14, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu,Mhe. Selemani Kakoso, wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyolenga kukagua mradi wa uundaji wa vichwa vya treni za MGR, unaoendelea katika karakana ya Pugu jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Kakoso kwa niaba ya kamati hiyo, ameitaka TRC kuhakikisha inawapa fursa na kuwapeleka vijana hao wenye ujuzi nje ya nchi kujifunza na kuchota utalaamu zaidi ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao, aidha alitoa rai kwa TRC kuwapa kipaumbele katika suala la ajira ili waendelee kulitumikia shirika na nchi kwa uaminifu.

Aidha,Mhe. Kakoso amesema, kamati inaipongeza kwa dhati TRC na Mkurugenzi wake Mkuu Mhandisi Machibya Shiwa, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia, Tanzania imefanikiwa kufanya hivyo kufuatia ucheleweshwaji wa vipuri kimkataba kutoka kwa wazabuni wa vipuri wa SMH kutokana na vita kati ya Ukraine na Urusi.
Hivyo, TRC ilifanya maamuzi ya kusafirisha vichwa viwili vilivyokamilika na kuundwa nchini Malaysia na kusafirisha vipuri kutoka kwa wazabuni kuja nchini na kuanza uundwaji wa vichwa sita vilivyobaki katika karakana ya Pugu.

Mhe. Kakoso ameongeza kuwa,uamuzi wa TRC kuunda vichwa vya treni hapa nchini umepunguza gharama kubwa ambayo serikali ingetumia kuagiza vichwa hivyo na pia imewezesha vijana wengi wa Kitanzania wenye ujuzi kuajiriwa.

Aidha,Mhe. Kakoso amewahimiza watumishi wa Shirika la Reli Tanzania kuwa wazalendo katika kulitumikia shirika na kutunza rasilimali zilizopo na kuepuka vitendo vya hujuma kwa shirika.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi,Mhe.David Kihenzile ameendelea kuipongeza Serikali kupitia TRC kwa kukuza sekta ya uchukuzi kwa kuendelea kujenga miundombinu bora na yenye ufanisi na kununua vitendea kazi ikiwemo vichwa na behewa.
"Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya uchukuzi, serikali imeendelea na ujenzi wa reli ya kisasa zaidi ya kilomita 2,290 na sasa inanunua vitendea kazi ili kuboresha sekta hii,"amesema Mhe.Kihenzile.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Mhandisi Machibya Shiwa pamoja na masuala mengine, aliiambia kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu juu ya manufaa ya mradi wa uundaji wa vichwa vya treni za MGR Daraja la 91XX katika karakana ya Pugu.

Amesema, ni pamoja na fursa za ajira amabpo jumla ya vijana 34 ambao hawakuwa wameajiriwa sasa wameajiriwa kupitia mradi huo.
"Kupitia mradi huo baadhi ya Watanzania, wamepata kuuza bidhaa zinazotumika katika uundaji wa vichwa hivyo nao ni kama wenye mashine za kuchonga vipuri, wauzaji wa vifaa ujenzi, boliti na nati, wauzaji vifaa vya umeme, mabomba, wauzaji vilainishi, bidhaa za mpira na nyinginezo,’’amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa TRC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here