PWANI-Jukwaa la Wanawake Viongozi nchini (WLF) limetoa msada wa vyerehani vitano nyenye thamani ya shilingi milioni 1.3 kwa Kikundi cha Wanawake cha Fountain of Joy cha Kibaha kwa Mbonde mkoani Pwani.
Mbali na vyerehani hivyo,pia WLF imedhamini mafunzo ya wajasiriamali kwa wanawake na vijana wa kikundi hicho,lengo likiwa ni kuhakikisha wanachama wa kikundi hicho wanapiga hatua kimaendeleo.
Akikabidhi vyerehani hivyo,Mwenyekiti wa WLF, Dkt. Eveline Munisi amesema kuwa,lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuhakiksha kuwa wanakiwezesha kikundi hicho ili kiweze kuongeza uzalishaji, mapato pamoja na stadi za kazi kwa wanachama wake.
Amesema kuwa,wanawake ni kundi kubwa ambalo halitakiwi kuachwa nyuma na kuongeza kwamba endapo litaachwa Tanzania haiwezi kupiga hatua kufikia Dira ya Maendeleo ya 2050.
"Wanawake ndio walezi wakubwa sana wa familia, sasa kwa hali yoyote ile wakiachwa nyuma mpango wa Dira ya Maendeleo 2050 haiwezi kufikiwa,hivyo ni muhimu sana wanawake pia washirikishwe kwenye kila hatua katika kuhakikisha wanapiga hatua za kimaendeleo," alisema.
Alisema kuwa, pamoja na mambo mengine WLF imetoa mafunzo ya afya ya akili na ya ujasiriamali ili wanawake na vijana waliopo kwenye kikundi hicho wananufaike na kwamba anaamini wakinufaika wao na watanufaisha na wengine zaidi.
Aidha, alitoa wito kwa wanawake na vijana kufuatilia na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza ili kupata maarifa na ujuzi mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Happy Wadelanga amesema kuwa, mbali na mafanikio, lakini kikundi chao kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa wakufunzi wa kutoa elimu ya ujasiriamali na ukosefu wa vitendea kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake cha Fountain of Joy, Deograsia Mwanyika ameishukuru WLF kwa msaada huo ambao utasaidia kikundi hicho katika masuala mbali mbali ya ushonaji ili waweze kuzalisha zaidi na kuwata Wanawake wasimuangushe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akifanya kazi Kwa juhudi kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Naye, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Muharakani, Ally Rwambo amesema, maendeleo hayana dini, itikadi wala kabila na ameishukuru sana WLF kwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi.
Amesema, elimu hiyo inahitajika sana kwa wananchi wote na kuwataka wasichoke kufanya hivyo Kwa wakati mwingine na kwamba uwanja upo wazi.
Jukwaa la WLF linaundwa na wanawake waliogombea nafasi ya Urais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2025.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa WLF, Azza Suleiman ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wanawake, vijana na makundi mbalimbali kwa kuwashika mikono.


