NA DIRAMAKINI
UZINDUZI wa jukwaa jipya la kidijitali la biashara ya madini lijulikanalo kama Tellus Minerals B2B unatarajiwa kufungua fursa mpya za masoko ya kimataifa kwa wachimbaji wadogo na wa kati nchini Tanzania, kwa kuwaunganisha moja kwa moja na wanunuzi, wawekezaji na wadau wa sekta ya madini duniani.
Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Tellus Minerals B2B, Idrissa Songoro akizungumza jijini Dar es Salaam amesema, jukwaa hilo limeanzishwa kwa lengo la kuleta mabadiliko katika biashara ya madini duniani kwa kutoa mazingira ya wazi na huru ya kidijitali yanayowawezesha wadau kuthibitishwa na kuwasiliana moja kwa moja bila kupitia kwa madalali.
Alieleza kuwa, kupitia mfumo huo, wachimbaji na wazalishaji wa madini wanaweza kuunganishwa moja kwa moja na wanunuzi wa kimataifa pamoja na wawekezaji, jambo litakalowawezesha kufanya majadiliano ya kibiashara kwa uwazi na kujenga ushirikiano endelevu.
Jukwaa hilo linakusudia kuwaleta pamoja wachimbaji, wazalishaji, wanunuzi wa viwandani, wafanyabiashara wa madini, wawekezaji, watengenezaji wa vifaa vya uchimbaji pamoja na serikali katika mfumo mmoja wa kidijitali.
Hata hivyo, mfumo huo hautahusika na malipo, huduma za dhamana ya miamala wala kutoza kamisheni; jukumu lake kuu ni kuwezesha wadau kuwasiliana na kufanya makubaliano yao binafsi.
Kwa mujibu wa Songoro, jukwaa hilo linaangazia hasa madini muhimu kama dhahabu, shaba, kobalti, lithiamu na madini adimu ya ardhini ambayo mahitaji yake yanaongezeka duniani kutokana na maendeleo ya viwanda na teknolojia.
Aliongeza kuwa,wachimbaji wadogo nchini Tanzania, hasa waliopo katika maeneo yenye utajiri wa madini, watanufaika zaidi kwa kuwa rasilimali zao zitapata fursa ya kuonekana moja kwa moja kwa wanunuzi, wasafishaji wa madini na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Songoro alibainisha kuwa, mpango huo pia unalenga kutatua changamoto zilizokuwepo kwa muda mrefu kwa wachimbaji wadogo, ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika, utegemezi kwa madalali na bei zisizo na ushindani katika soko la kimataifa.
“Wachimbaji wadogo mara nyingi hukosa fursa ya kuonekana katika soko la kimataifa. Kupitia jukwaa hili wataweza kuwasilisha rasilimali zao zilizothibitishwa moja kwa moja kwa wadau wa kimataifa na kujadiliana bei yenye manufaa zaidi,” alisisitiza.
Mbali na kuwasaidia wachimbaji, mfumo huo pia utaziwezesha serikali na taasisi za udhibiti kushiriki taarifa muhimu kama sera za sekta ya madini, vivutio vya uwekezaji, taarifa za kijiolojia na mifumo ya udhibiti ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya madini nchini.
Aidha, jukwaa hilo linatarajiwa kuandaa semina na mijadala ya kimtandao kuhusu mwenendo wa soko la madini duniani, maendeleo ya minyororo ya thamani pamoja na fursa mpya za uwekezaji. Kwa sasa, usajili kwa wadau unapatikana bure hadi Julai 27, 2026.
Katika hatua nyingine, mkutano wa kimtandao unaotarajiwa kufanyika Aprili 10, 2026 ambapo utawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutoka duniani kote ili kujadili mwenendo wa soko na fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
Songoro amesema,katika ulimwengu wa sasa, biashara ya madini inahitaji kufanyika kwa uwazi na ushindani wa kimataifa ili kuhakikisha thamani halisi ya rasilimali hizo inapatikana.
Kupitia jukwaa hili jipya la kibiashara, wafanyabiashara watawezeshwa kufanya biashara ya madini kwa kuzingatia bei shindani katika soko la dunia badala ya kutegemea maamuzi ya mtu mmoja au kikundi kidogo katika upangaji wa bei.
Pia,hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwazi katika shughuli za biashara ya madini, huku ikitoa fursa kwa wanunuzi na wauzaji kushiriki moja kwa moja katika soko lenye ushindani wa haki.
Mfumo huo pia utarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za masoko, hali itakayowezesha wafanyabiashara kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara.
Aidha, jukwaa hilo linatarajiwa kuwasaidia wafanyabiashara wa ndani kufanya biashara kwa urahisi zaidi, jambo litakalochochea ukuaji wa biashara za ndani na kuimarisha ushiriki wao katika masoko ya kimataifa.
Kupitia mfumo huo, taratibu za biashara zitakuwa rahisi na zenye ufanisi zaidi, hivyo kurahisisha shughuli za uuzaji na ununuzi wa madini ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Serikali inatarajiwa kuweka sera, kanuni na miongozo itakayohakikisha matumizi sahihi ya jukwaa hilo pamoja na kulinda maslahi ya wadau wote katika sekta ya madini ambazo Songoro amesisitiza kuwa, Serikali inakaribishwa katika jukwaa hili muhimu.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za madini, kuongeza mapato ya taifa na kuchochea maendeleo ya uchumi kwa ujumla.
Tags
Fursa katika Madini
Habari
Idrissa Songoro
Masoko ya Madini
Sekta ya Madini
Tellus Minerals B2B
