DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Sauda Msemo, amesema mifumo ya malipo ina mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.
Bi. Msemo amesema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Bi. Lucy Shaidi, wakati wa ufunguzi wa kikao cha pamoja cha usimamizi wa mifumo ya malipo na ulipaji kwa nchi za Afrika Mashariki, kilichofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi 2026.
Amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuboresha mifumo ya malipo kutoka njia za zamani hadi mifumo ya kisasa ya kidijitali inayowezesha miamala kufanyika kwa haraka na kwa ufanisi.
Ameeleza kuwa,mifumo hiyo ni pamoja na mfumo wa malipo ya miamala mikubwa baina ya benki (TISS), mfumo wa malipo madogo na makubwa (TACH), pamoja na mfumo wa malipo ya papo kwa hapo (TISS). Aidha, huduma za fedha kwa njia ya simu zimeendelea kupanuka na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kiuchumi za kila siku.
Katika ngazi ya kikanda, Bi. Msemo ametaja mafanikio yaliyopatikana kupitia Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS) unaowezesha miamala ya kuvuka mipaka kwa kutumia sarafu za ndani, pamoja na hatua za kupokea viwango vya kimataifa ikiwemo ISO 20022 ili kuboresha ushirikiano wa mifumo.
Akizungumzia umuhimu wa zoezi la pamoja la usimamizi, alisema ni jukwaa muhimu linalosaidia kuimarisha usimamizi wa mifumo ya malipo kati ya nchi wanachama, kujenga uwezo kupitia kujifunza kwa pamoja, na kushughulikia hatari zinazoibuka katika mifumo ya kifedha inayozidi kuwa ya kidijitali na kuunganishwa.
Ameongeza kuwa, maeneo ya mkazo kwa mwaka huu, yakiwemo usimamizi unaozingatia vihatarishi, uzingatiaji wa sheria za kupambana na utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi (AML/CFT/CPF), ufuatiliaji wa miamala na utawala bora, ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti na usimamizi chini ya Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015, sambamba na kuhamasisha ubunifu kupitia programu kama Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha (FinTech Regulatory Sandbox).

