ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kilimo cha mwani kinaongezewa thamani ili kuwanufaisha wakulima wa zao hilo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 30 Machi 2026, alipokutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya TSC Purple Limited ya India, Dkt. Stefan Kraan, pamoja na ujumbe wake waliofika Ikulu, Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameueleza ujumbe huo kuwa lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa zao la Mwani, kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika pamoja na bei nzuri kwa wakulima wa mwani.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameishauri Kampuni ya TSC Purple Limited kuweka utaratibu wa kununua mwani ukiwa mbichi moja kwa moja kutoka kwa wakulima, hatua itakayosaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kampuni ya TSC Purple Limited, Dkt. Stefan Kraan, amesema kampuni hiyo inaendelea na ufungaji wa mitambo katika kiwanda cha kusarifu mwani kilichopo Chamanangwe, ambapo kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026 na uzalishaji kuanza rasmi mwezi Septemba 2026.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mwani Zanzibar, ikiwemo uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kama mbolea, chakula cha mifugo na dawa.
Vilevile, Dkt.Kraan amemueleza Rais Dkt. Mwinyi kuwa kampuni hiyo inatarajia kuandaa mkutano mkubwa wa wadau wa kilimo cha mwani utakaofanyika Tanzania kuanzia tarehe 16 hadi 19 Juni 2026, pamoja na kufanya ziara maalum katika maeneo ya uzalishaji wa mwani Zanzibar kwa lengo la kubaini fursa mpya za kuendeleza sekta hiyo.




