Mahakama Kuu yaamuru kufungwa kwa Kampuni ya Sahara Media Group kutokana na madeni

MWANZA-Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara imeamuru kufungwa kwa kampuni ya Sahara Media Group Limited, iliyokuwa ikijishughulisha na shughuli za vyombo vya habari, matangazo pamoja na huduma za uchapishaji nchini Tanzania, kufuatia kushindwa kumudu hali yake ya kifedha. Sahara Media Group ni wamiliki wa Star TvRFA na Kiss FM kutoka Ilemela jijini Mwanza.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji, Dkt. Mwajuma Kadilu baada ya kuridhia ombi la kufilisi kampuni hiyo lililowasilishwa na kampuni yenyewe, ikieleza kuwa imekumbwa na matatizo makubwa ya kifedha yanayoifanya ishindwe kulipa madeni yake.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, ombi hilo liliungwa mkono na kiapo cha Afisa Mkuu wa kampuni hiyo, Steven Diallo, pamoja na vielelezo mbalimbali ikiwemo Memorandum na Articles of Association za kampuni, azimio la Bodi ya Wakurugenzi, notisi za madai ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mwanza, na taarifa za fedha zilizokaguliwa za miaka ya 2023 na 2024.

Katika uamuzi wake, Jaji Kadilu alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani umeonyesha wazi kuwa kampuni hiyo imepata hasara kubwa ya kifedha na haina tena uwezo wa kulipa madeni yake.

“Mahakama imeridhika kuwa mwombaji amepata hasara kubwa na hana uwezo wa kulipa madeni yake. Hivyo, hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ni kufungwa kwa kampuni hiyo,” alisema Jaji Kadilu katika uamuzi wake.

Mahakama pia imeteua mawakili Alex Mgongolwa wa kampuni ya uwakili ya Excellent Attorneys na Frank Mwalongo wa Apex Attorneys kuwa wasimamizi wa pamoja wa mchakato wa kufilisi kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni, wasimamizi hao watasimamia mchakato huo kwa kipindi cha miezi mitatu chini ya uangalizi wa mahakama, ikiwa ni pamoja na kuchukua udhibiti wa mali zote za kampuni, kusimamia ulipaji wa madeni na kuwasilisha ripoti ya mwisho mahakamani baada ya kukamilika kwa zoezi hilo.

Aidha, mahakama imepiga marufuku uhamishaji wa mali za kampuni, uhamishaji wa hisa au mabadiliko yoyote ya wanachama wa kampuni kuanzia kuanza kwa mchakato wa kufungwa kwa kampuni hiyo.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani umebainisha kuwa kampuni hiyo inadaiwa takribani shilingi milioni 97.7 za kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku taarifa za fedha zikionyesha kuwa kampuni ilipata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 3.9 mwaka 2023 pamoja na hasara nyingine katika miaka iliyotangulia.

Aidha, ilielezwa mahakamani kuwa takribani asilimia 80 ya mapato ya kampuni hiyo yalikuwa yakitumika kulipa madeni ya kodi, hali iliyosababisha kushindwa kuendesha shughuli zake za kawaida na kutimiza majukumu yake ya kifedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here