KIGOMA-Machi 2,2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mheshimiwa Maila M.Makonya (PRM) na Mwendesha Mashtaka kutoka TAKUKURU, Bw. Balamu Kisumo, limefunguliwa shauri la uhujumu uchumi Namba ECO.4485/2026 kati ya Jamhuri dhidi ya Bw.Perfect Slaa Heke (36) ambaye alikuwa muuguzi katika Zahanati ya Kisogwe.
Mshtakiwa anakabiliwa na kosa la ubadhirifu na ufujaji kinyume na kifungu cha 28(1) PCCA sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022,baada ya mshtakiwa kufanya ubadhirifu wa dawa za binadamu zenye thamani ya shilingi 5,381,379.069.
Kwamba, mshtakiwa wakati akiwa muuguzi na mtunza dawa katika Zahanati ya Kisogwe alikuwa anaomba dawa kwenye zahanati mbalimbali ambazo aliziomba kwa matumizi ya zahanati hiyo, lakini alikuwa anatumia dawa hizo kwa maslahi yake binafsi.
Baada ya kusomewa shtaka lake, Mshtakiwa alikana shtaka na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya mahakama.
Shauri limepangwa tena Machi 13,2026 kwa ajili ya uwasilishaji wa hoja za awali (PH).
