Profesa Shemdoe aelekeza maafisa wanaosimamia Mradi wa Lishe kupatiwa usafiri

GEITA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, Mheshimiwa Prof.Riziki Shemdoe ameelekeza Maafisa Lishe na Maendeleo ya Jamii wanaosimamia utekelezaji wa Mradi Jumuishi wa Lishe katika Mkoa wa Geita, Tabora na Iringa kupatiwa vyombo vya usafiri ili waweze kwenda kutoa huduma kwenye maeneo yanayokabiliwa na matatizo ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Prof. Shemdoe ametoa maelelezo hayo Machi 03, 2026, wakati akizindua Mradi Jumuishi wa Lishe katika Mkoa wa Geita, ambao utawawezesha watoto wa mkoa wa Geita kukua vizuri kimwili na kiakili, na kuwa na nguvu na afya bora.

“Katibu Mkuu na wataalam mnaosimamia mradi huu, hakikisheni kupitia bajeti za mradi mnawapatia Maafisa Lishe na Maendeleo ya Jamii vyombo vya usafiri katika halmashauri zote zinazotekeleza mradi huu ili waweze kutoka sehemu moja kwenda nyingine kuwahudumia watoto,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amesema, kipekee anashukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake ambazo zimewezesha kupatikana kwa mradi huo jumuishi wa lishe, “Mwaka 2022 akiwa Jijini Washington, nchini Marekani akihudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alikutana na kukubaliana na Mama Jamie Cooper, Rais wa Taasisi ya Big Win Philanthropy kuanzisha ushirikiano uliowezesha kupatikana kwa mradi huu”.

Mkuu wa Mkoa wa Geita,Mhe. Martine Shigela amemshukuru Mhe. Rais kwa kuelekeza na kuhakikisha kwamba kila kijiji kuna kuwa na siku ya afya na lishe na amemhakikishia Prof. Shemdoe kuwa mkoa wake utaendelea kutekeleza kampeni hiyo ya siku ya afya na lishe ili kupunguza changamoto ya utapia mlo.
Naye, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI anayeshughulikia afya, Prof. Tumaini Nagu, amesema Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ina imani kubwa kuwa, ushirikiano thabiti wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wa mikoa ya Geita, Tabora na Iringa utawezesha kufikia malengo ya mradi jumuishi wa lishe ambao umezinduliwa na Prof. Shemdoe.

Pia, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Mohammed Gombati amesema kuwa, kama lililivyo jina la mradi jumuishi, wamekusanyika watumishi kutoka idara zote ili kwa pamoja waweze kujipanga katika kutekeleza mradi huo jumuishi wa lishe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Bw. Luitfrid Nnally amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika suala la lishe kwa kuleta mkataba wa lishe tangu akiwa Makamu wa Rais, kitendo ambacho kimepelekea Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoa kipaumbele katika suala la lishe.

Taasisi ya Big Win Philanthropy ya Nchini Uingereza inafadhili Mradi huo Jumuishi wa Lishe, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na matatizo ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here