MOROGORO-Jamii imetakiwa kushughulikia masuala ya maji na jinsia kwa pamoja ili kufungua njia za uwezeshaji, usawa, na maendeleo endelevu katika upangaji na utekelezaji wa miradi na sera ya Sekta ya Maji.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe.Angellah Kairuki (Mb) ametoa wito huo mjini Morogoro kwenye ufunguzi wa Mdahalo wa Wadau kuhusu Maji na Jinsia ulioandaliwa na Wizara ya Maji ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji.
Mhe.Kairuki amesema maji yanatunza mazingira pamoja na kaya, yanasaidia kilimo, yanabeba viwanda.
Ameainisha kuwa bila majisafi na salama jamii haiwezi kustawi, uchumi hauwezi kukua, na mazingira hayawezi kuendelea hivyo jamii inalo jukumu kubwa la utayari kwa kila mmoja.
Amesisitiza kuwa Serikali imetambua umuhimu wa maji na kuifanya kuwa moja ya agenda za vipaumbele muhimu katika jitihada za kuboresha maisha ya wananchi, na imeendelea kuweka mikakati na kuimarisha uwekezaji katika sekta ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema Wizara ya Maji imejipanga kuhakikisha inatoa majibu ya changamoto zote zinazowakumba wananchi kwa jinsia zote katika upatikanaji wa majisafi na salama.
Amesema Wizara ya Maji inatambua kuwa changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama bado inaathiri makundi mbalimbali katika jamii kwa namna tofauti, hususan wanawake na wasichana ambao hubeba jukumu kubwa la kutafuta na kusimamia matumizi ya maji katika ngazi ya familia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga amesema kamati anayoiongoza ipo tayari kupokea mawazo ya wadau na kuyafanyia kazi.“Kazi kubwa ya Bunge ni kutunga Sheria, kuisimamia Serikali, na kuwawakilisha wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania. Hivyo, ni matumaini yetu kuwa kupitia Mdahalo huu tutapata mapendekezo yenu kuhusu maeneo muhimu ya kuzingatia wakati wa utungaji wa sheria ili kuhakikisha kuwa masuala ya kijinsia yanazingatiwa ipasavyo.” Mhe. Kiswaga amesema.
Wizara ya Maji inaadhimisha Wiki ya Maji ambayo inaanza tarehe 16 hadi 22 Machi ambayo ni Siku ya Maji Duniani.

