RUVUMA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia rai wa kigeni aitwaye Wang Renbiao (28) ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Mkuzo mjini Songea, kwa kosa la kukutwa akiwa na mashine bandia 60 za michezo ya bahati nasibu.
Akithibitisha hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G. Chilya amesema kuwa Machi 24,2026 majira ya saa nne asubuhi huko maeneo ya Mkuzo Manispaa ya Songea, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha.
Sambamba na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walimkamata mtuhumiwa huyo akiwa na jumla ya mashine 60 za michezo ya bahati nasibu ambazo alikuwa amezihifadhi stoo kwa ajili ya kuzisambaza.
Ni katika maeneo mbalimbali ya starehe katika vijiji vya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na baada ya kuzikagua ilibainika kuwa,mashine hizo ziliingizwa nchini kinyume cha sheria.
Pia,mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa na risiti feki za mashine hizo pamoja na stika nyingine za Cleopatra Gaming Tanzania L.t.d ambazo pia zilibainika kughushiwa kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Amesema, kutokana na operesheni na misako inayoendelea kufanyika maeneo yote mkoani Ruvuma, Jeshi la Polisi tarehe 25 Machi,2026 Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa tisa, majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kipelelezi ambao walikuwa wakijihusisha na unyang'anyi na wizi wa pikipiki maeneo mbalimbali mkoani Ruvuma.
Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika kwa hatua zaidi.



