Meli nne za mizigo zakaribia kukamilika Karema,kuimarisha biashara Ziwa Tanganyika

KAREMA-Meli kubwa nne za mizigo zilizojengwa katika Bandari ya Karema, ambazo ziko katika hatua ya mwisho ya ujenzi, zimefikia asilimia 95 ya kukamilika.
Kwa sasa, meli hizo zinapata ukaguzi wa mwisho majini kabla ya kuanza shughuli zake rasmi.

Kwa mujibu wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, meli hizi zinazojengwa kwa ushirikiano wa kampuni ya Gold Voyage Logistics ya Zijin Mining, zitakuwa na uwezo wa kubeba tani 8,000 kila moja.

Aidha,meli hizo zitatumika kukuza biashara katika Ziwa Tanganyika na kuimarisha mawasiliano ya kibiashara kati ya Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Burundi.

Meli hizi zitachochea ukuaji wa uchumi kwa kusafirisha kwa ufanisi madini na mazao ya kilimo, huku pia zikileta manufaa makubwa kwa jamii.

Pia, meli hizo zimejikita katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano, kuunda ajira za ndani, na kukuza maendeleo katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma.

Karema ni miongoni mwa bandari kuu ya kisasa katika ukanda wa maziwa makuu nchini iliyopo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi Mkoa wa Katavi ikiwa na umbali wa kilomita 120 kutoka mji wa Mpanda mkoani humo.

Sambamba na kilomita 110 kutoka Barabara Kuu ya Mpanda kwenda Kigoma ambayo imejengwa kisasa kulinganisha na bandari nyingine za mwambao wa ziwa hilo.

Bandari hii ambayo ni miongoni mwa bandari 17 za Ziwa Tanganyika ina ukubwa wa eneo la ekari 66 kwa jumla ikiwa na miundombinu ya kisasa kulinganisha na bandari nyingine za Ziwa Tanganyika na ndiyo bandari pekee iliyo jirani zaidi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Bandari ya Kalemie ambayo ni bandari maarufu ya nchi hiyo.

Pia,Karema ni miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyotekelezwa na Serikali yenye lengo la kufungua lango la biashara kati ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Tanzania lengo likiwa kupunguza utegemezi wa kulifikia soko kubwa la DRC kupitia nchi ya Zambia.

Hii ni hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha biashara na usafirishaji wa bidhaa katika eneo la Ziwa Tanganyika, na kuleta fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here