Siku zahesabika ukomo usajili wa hiari wanaokusanya taarifa binafsi Tanzania

NA DIRAMAKINI

TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini (PDPC) imetoa onyo la mwisho kwa taasisi zote zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi kujisajili kabla ya Aprili 8, 2026 huku ikibainisha kuwa, hatua kali za kisheria zitaanza kuchukuliwa kuanzia Aprili 9,mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa PDPC,Dkt.Emmanuel Lameck Mkilia ameyasema hayo Machi 26,2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amefafanua kuwa, Serikali imetoa muda wa kutosha tangu mwaka 2024 kwa taasisi kujisajili ikiwa ni pamoja na kuongeza muda huo mara mbili.

Amesema, kuanzia Aprili 9,mwaka huu utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Sura ya 44 utaanza rasmi, na taasisi au mtu yeyote atakayebainika kutokujisajili atachukuliwa hatua za kisheria.

Dkt.Mkilia amesema,Serikali ilitoa muda wa kutosha wa kujisajili ambapo ulianza Aprili, 2024 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipozindua Tume.

Aidha, amesema muda uliongezwa mara mbili, mara ya mwisho ikiwa ni uamuzi wa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ambaye aliweka tarehe ya mwisho kuwa Aprili 8, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, adhabu kwa mtu binafsi ni faini ya kuanzia shilingi 100,000 hadi milioni 20 au kifungo cha hadi miaka 10 jela.

Aidha,kwa upande wa taasisi na makampuni, adhabu ni faini kuanzia shilingi milioni moja hadi shilingi bilioni tano za kitanzania, kulingana na aina ya ukiukwaji.

Vilevile, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inazigusa sekta zote muhimu zikiwemo wizara na idara za Serikali, mabenki, kampuni za bima, hospitali, shule, vyuo, kampuni za simu, viwanda na sekta ya utalii.

Nyingine ni hoteli, kampuni za usafirishaji, kampuni za ujenzi, vyama vya siasa, vyama vya wafanyakazi, jumuiya za kidini, mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi nyingine nyingi.

Sheria hii ni ngao kwa mwananchi ambaye ndiye muhusika wa taarifa, kwani inalinda haki ya msingi ya faragha.

Pia, inajenga imani kati ya watoa huduma na wateja wao, jambo ambalo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa kidigitali na uwekezaji nchini.

Kuhusu PDPC

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini, ilianzishwa rasmi Mei 1, 2023 kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na.11, 2022.

PDPC ilianza utekelezaji wa majukumu yake kama matokeo ya utekelezaji wa sheria hiyo na kuanzishwa rasmi majukumu yake.

Septemba 12, 2021 kupitia Hati ya Mgawanyo wa Majukumu iliyotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na.782 la Novemba 22,2021 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliundwa ambapo pamoja na majukumu mengine wizara ilipewa jukumu la kusimamia Ulinzi na Usalama wa Mitandao nchini.

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni nyenzo mtambuka muhimu katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa hasa katika kipindi hiki cha Mapinduzi ya 4, 5 na 6 ya Viwanda.

Pamoja na mafanikio yanayotokana na ukuaji wa TEHAMA duniani pia kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo ulinzi wa taarifa binafsi ambazo zimekuwa zikikusanywa, zikichakatwa na wakati mwingine kusafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine bila kuzingatia utaratibu na misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyokubalika duniani.

Tanzania ni mwanachama wa jumuiya mbalimbali za Kikanda na Kimataifa zikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU).

Kwa kuwa suala la mitandao halitambui mipaka ya kijiografia, nchi wanachama wa jumuiya hizo zimekubaliana kuwa na Sheria mahususi na Taasisi Huru katika kukabiliana na changamoto hizo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki iliandaa Mwongozo wa Sheria za Usalama wa Mtandao mwaka 2008, Jumuiya ya SADC iliandaa Sheria tatu za mfano za Usalama Mtandao za mwaka 2012 na Umoja wa Afrika iliandaa Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Usalama Mtandao na Ulinzi wa Taarifa Binafsi pia maarufu kama Mkataba wa Malabo wa mwaka 2014.

Mikataba na Miongozo hiyo kwa pamoja inazitaka nchi wanachama kuwa na Sheria tatu za msingi za usalama wa mtandao na Taasisi huru, Sheria hizo ni Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambayo itaanzisha Tume huru ya kusimamia ulinzi wa taarifa binafsi.

Pia, nchi za Ulaya nazo zimeandaa Mwongozo wa kukabiliana na changamoto hizo. Takwimu zinaonesha kuwa,nchi mbalimbali zimetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kama ambavyo imebainishwa.

Nchi 162 kati ya nchi 198 Duniani zimetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Nchi 36 kati ya nchi 54 za Afrika tayari zimetunga Sheria hiyo. Nchi 12 kati ya nchi 16 za SADC zimeshatunga Sheria hiyo.

Nchi 4 kati ya nchi 6 za EAC zimetunga Sheria hiyo. Nchi ya Burundi na Sudani ya Kusini ziko kwenye mchakato wa kutunga sheria hii.

Tanzania imekamilisha uandaaji wa Sheria hizo tatu za msingi ambazo ni Sheria za Makosa ya Mtandao 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, 2015 na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa ya mwaka 2022.

Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na.11 ya mwaka 2022 ni Sheria muhimu kwa Taifa letu kwani ni Sheria ambayo inaweka utaratibu wa kulinda haki ya faragha ya Mtu kama ambavyo imebainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 16 (1)(2) na Ibara ya 15 ya Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katiba zote mbili zinazungumzia haki ya faragha na usalama wa mtu "Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake binafsi".

Pia, ibara hizo, zimeainisha wajibu wa Serikali ambapo imeelezwa kuwa "kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kwa mujibu wa Katiba, Mamlaka itaweka utaratibu wa sheria kuhusu hali, namna na kiasi ambacho haki ya mtu na faragha na usalama wa nafsi yake, mali yake na maskani yake yanaweza kuingiliwa bila kuathiri ibara hii".

Kuwepo kwa Sheria hii, ni utekelezaji matakwa ya Katiba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Ibara ya 61(b) ambayo imeelekeza kuongeza ufanisi na usiri wa Taarifa za wananchi katika mawasiliano kwa kutunga Sheria ya kuimarisha ulinzi wa taarifa na takwimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here