DODOMA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S.Johari leo Machi 13, 2026 ameapishwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, katika hafla fupi ya uapisho iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jijini Dodoma.
Mhe. Johari ameapa mbele ya Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George M. Masaju, kufuatia kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume hiyo.Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameteuliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mara ya pili na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Novemba, 2025.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameapishwa kuwa Kamishna kutimiza takwa la Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 Sura ya 237 inayomtaka kila Kamishna kuapishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake.
Sambamba na Mhe. Johari, Wajumbe wengine wa Tume ya Utumishi wa Mahakama walioapishwa ni pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Gerson Mdemu, na Mawakili wa Kujitegemea Bw. Thomas Nyanduga na Bi. Dorcas Mutabuzi.




