DAR-Muhubiri na mwinjilisti wa kimataifa, Dkt. Alphonce Temba amempongeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Profesa Alhad Mussa Salum, kwa juhudi zake za kuimarisha maridhiano na amani nchini.
Muhubiri na mwinjilisti wa kimataifa, Dkt. Alphonce Temba (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Profesa Alhad Mussa Salum.Ni Machi 19, 2026 katika Ukumbi wa Police Mess, Oysterbay jijini Dar es Salaam baada ya hafla ya Iftar iliyoandaliwa na JMAT.
Akizungumza baada ya hafla ya Iftar ya pamoja iliyofanyika Machi 19, 2026 katika Ukumbi wa Police Mess, Oysterbay jijini Dar es Salaam, Dkt. Temba alisema kuwa,uongozi wa Sheikh Salum unaakisi maono mapana yenye mchango mkubwa si tu kwa Tanzania bali pia kwa Afrika na dunia kwa ujumla.
Alisema kuwa,maono hayo ni ya kipekee, kwani mataifa mengi duniani bado yanakumbwa na migogoro ya kidini, hususan kati ya waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo.
Aliongeza kuwa, baadhi ya nchi zimekumbwa na matukio ya chuki, ugaidi na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyochochewa na tofauti za kidini.



“Zipo nchi ambazo zimefikia hatua ya kushindwa kupata suluhu ya kudumu kutokana na migogoro ya kidini, mfano Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hali kama hiyo pia inaonekana nchini Nigeria na maeneo mengine,” alisema Dkt. Temba.
Aidha, alisisitiza kuwa juhudi zinazofanywa na JMAT chini ya uongozi wa Sheikh Salum zinapaswa kuungwa mkono na Serikali, pamoja na kupanuliwa katika ngazi za kikanda, hususan ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ili kuimarisha mshikamano na kupunguza chuki miongoni mwa mataifa wanachama kama Kenya na Uganda.
Alieleza kuwa juhudi hizo zinapaswa pia kufikishwa katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), akipendekeza uwepo wa mwakilishi kutoka JMAT atakayeshiriki kutoa elimu na uzoefu kuhusu maridhiano na ujenzi wa amani katika majukwaa ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Dkt. Temba, dunia ya sasa inahitaji ajenda zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi, hasa katika nyanja za kiuchumi na kimaadili.
Alisisitiza umuhimu wa kudumisha misingi ya utamaduni na maadili ili kujenga jamii yenye hofu ya Mungu, heshima na upendo.





“Ndani ya JMAT utakutana na viongozi wa dini mbalimbali wakiwemo maaskofu, masheikh, mitume, manabii, maimamu, wachungaji na wainjilisti wakikaa pamoja kujadili masuala ya amani huku wakitanguliza maslahi ya taifa. Haya si mambo madogo, bali ni maono makubwa yanayopaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania,” alisisitiza.
Hafla hiyo ya Iftar iliwaunganisha viongozi wa dini tofauti, wawakilishi wa Serikali, mabalozi, wanasiasa pamoja na watu mashuhuri, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mshikamano na kuimarisha amani nchini.
Mwinjilisti Dkt.Temba amezunguka zaidi ya matifa 12 duniani na amejionea mengi , ambayo yanampa nguvu ya kutamka wazi kuwa JMAT imebeba maono ya kidunia katika Ulimwengu wa sasa.
Tags
Dr Alphonce Boniface Temba
Habari
Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT)
Sheikh Profesa Alhad Mussa Salum
