DAR-Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kwaniaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kampuni ya MOTISUN Group, Bw. Ratish Kamania, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo pamopja na mambo mengine walijadili kwa kina kuhusu nafasi na mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi, hususan kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa vifaa vya ujenzi unaochochea maendeleo ya miundombinu.

Aidha, Mhe. Luswetula alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana, huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.
Kwa upande wake, Bw. Kamania alieleza dhamira ya kampuni yake kuendelea kupanua uwekezaji nchini, hatua itakayochangia kuongeza ajira, kukuza ujuzi wa vijana na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika maendeleo ya Taifa.




