Polisi Iringa wavunja mtandao wa wizi,pikipiki 115 zakamatwa

IRINGA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limefanikiwa kuvunja mtandao mkubwa wa wizi wa pikipiki uliokuwa ukifanya shughuli zake katika mikoa mbalimbali nchini, baada ya kukamata jumla ya pikipiki 115, watuhumiwa tisa pamoja na mali nyingine zinazodaiwa kupatikana kwa njia ya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema, mafanikio hayo yametokana na operesheni maalum iliyofanyika Januari 17, 2026 katika eneo la Kihesa, Manispaa ya Iringa.

Amesema,operesheni hiyo imewezesha kubainika kwa mtandao mpana uliokuwa ukijihusisha na wizi wa pikipiki katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro pamoja na maeneo mengine ya nchi.

“Haya ni mafanikio makubwa katika juhudi za Jeshi la Polisi za kupambana na vitendo vya uhalifu,” amesema Bukumbi.

Katika operesheni hiyo ya awali, watuhumiwa watatu waliotajwa kwa majina ya Ernest Mgaya, Oscar Malinda na Emilio Mfilinge walikamatwa wakiwa na pikipiki tatu zinazodaiwa kuibwa katika Mkoa wa Dodoma.

Kamanda Bukumbi ameeleza kuwa, baada ya kufanyiwa mahojiano, watuhumiwa hao walikiri kuhusika katika wizi wa zaidi ya pikipiki 50 kila mmoja, pamoja na kutengeneza kadi bandia zilizokuwa zikiuzwa kwa washirika wao waliopo Makambako.
Uchunguzi zaidi uliofanywa na Jeshi la Polisi ulipelekea kufanyika kwa msako katika mji wa Makambako, ambapo watuhumiwa wengine wawili, James Mgaya (29) na Jackson Chaula (28), walikamatwa wakidaiwa kuwa wanunuzi wakuu wa pikipiki hizo.

Katika upekuzi uliofanyika, polisi walifanikiwa kukamata pikipiki 82, guta moja, vibao 19 vipya vya namba za usajili, kadi bandia 50 za pikipiki, mashine ya kuoshea magari pamoja na kiasi cha shilingi 6,430,000.

Aidha, Kamanda Bukumbi amebainisha kuwa, mtandao huo unadaiwa pia kuhusisha watu wanaofadhili shughuli hizo za uhalifu katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Mbeya na Arusha.

Alitoa wito kwa wananchi wote waliopoteza pikipiki zao kufika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Iringa kwa ajili ya utambuzi wa mali zao, huku akisisitiza kuwa operesheni hiyo bado inaendelea.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mali zilizokamatwa katika operesheni hiyo ni pamoja na pikipiki 115, watuhumiwa tisa, gari moja, bajaj moja, guta moja, mashine ya kuoshea magari na vifaa vingine vinavyohusishwa na mtandao huo wa uhalifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here