RITA yapokea madai 248 mchakato wa ufilisi wa Kampuni ya Pride Tanzania

DAR-Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umepokea jumla ya madai 248 kutoka kwa wadau na taasisi mbalimbali kuhusiana na iliyokuwa kampuni ya utoaji mikopo ya Pride Tanzania, hatua inayolenga kuchakata, kuthibitisha na kutoa ufafanuzi juu ya uhalisia wa madai hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kabidhi Wasihi Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, alisema kuwa wakala huo uliteuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, kusimamia mchakato wa ufilisi wa taasisi hiyo ya kifedha. 

Alieleza kuwa, miongoni mwa majukumu waliyopewa ni kukusanya na kuhakiki taarifa sahihi za wadai na wadaiwa wa kampuni hiyo.

“Mnamo Novemba 7, 2025, tulipokea uteuzi rasmi kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, kupitia maombi namba 2272 ya mwaka 2025, kuwa mfilisi wa kampuni ya Pride,” alisema Bw. Kanyusi.

Alifafanua kuwa kufuatia uteuzi huo, Januari 26, 2026, RITA ilitoa notisi kwa umma ikiwataka wadai wote kuwasilisha madai yao pamoja na vielelezo vya uthibitisho ndani ya siku 14, kuanzia tarehe ya notisi hadi Februari 8, 2026.

Kwa mujibu wa Bw. Kanyusi, katika kipindi hicho cha majuma mawili, wakala umepokea madai 248 kutoka kwa makundi mbalimbali yakiwemo wafanyakazi, taasisi za kifedha pamoja na vikundi vingine vya kijamii na kiuchumi.

Alibainisha kuwa kati ya madai hayo, madai 111 yanatoka kwa wafanyakazi, yakihusisha malimbikizo ya mishahara, stahiki za usafiri na madai mengine yanayohusiana na ajira. Aidha, taasisi tisa za zabuni zimewasilisha madai ya malipo ya huduma na vifaa walivyotoa kwa kampuni hiyo katika shughuli zake za kila siku.

Hata hivyo, Bw. Kanyusi alieleza kuwa madai 70 kati ya yaliyopokelewa hayakubainisha wazi aina ya madai husika, kinyume na utaratibu uliowataka wadai kueleza kwa kina wanachodai na kuambatanisha ushahidi stahiki.

“Tumepokea pia madai ambayo hayajaeleza kwa uwazi aina ya madai yao. Hivyo, tutaendelea kuyafanyia kazi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha haki inatendeka,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa licha ya baadhi ya wadai kushindwa kuwasilisha madai yao ndani ya muda uliotolewa, RITA itaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini wadai wote wa kampuni hiyo na kuhakikisha mchakato wa ufilisi unatekelezwa kwa uwazi na ufanisi.

Kwa mujibu wa taarifa za kihistoria, kampuni ya Pride Tanzania ilisajiliwa rasmi Mei 5, 1993, ikiwa na dhamira ya kutoa mikopo isiyo na dhamana kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo, hususan vijijini, kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here