IRINGA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limekamata vifaranga vya kuku vilivyokuwa vikisafirishwa kwenye mabasi mawili ya abiria yakitokea mpakani mwa nchi jirani ya Malawi kuelekea Visiwani Zanzibar, baada ya kubaini kasoro kwenye nyaraka za usafirishaji.
Akizungumza na vyombo vya habari katika kituo kikubwa cha Polisi mkoani humo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, amesema kuwa idadi ya vifaranga iliyoainishwa kwenye nyaraka rasmi ilikuwa tofauti na idadi halisi iliyokutwa ndani ya mabasi hayo, hali iliyozua mashaka na kusababisha kukamatwa kwa mzigo huo kwa uchunguzi zaidi.
Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa wafanyabiashara na wasafirishaji kuzingatia sheria na taratibu za usafirishaji wa bidhaa, likisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka sheria hizo.
